Watu tisa wamefariki dunia, wakiwemo wanafunzi wanne, huku wengine 16 wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Kambi ya Nyasa, wilayani Chemba, mkoani Dodoma.
Ajali hiyo imehusisha basi la abiria aina ya Tata mali ya Kampuni ya Babuu Trans lenye namba za usajili T129 DVX na lori la mizigo aina ya Fuso lenye namba T907 EJZ.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka husika, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori, ambaye alielezwa kuwa alipoteza mwelekeo na kuingia upande wa basi, na kusababisha ajali hiyo mbaya.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema mkoa umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo.
“Ajali hii ilisababisha vifo vya watu watano papohapo na majeruhi 20. Wakati wakiendelea kupatiwa huduma, wanne kati ya majeruhi hao walifariki dunia wakiwa njiani kuhamishiwa hospitali ya rufani, na kufanya idadi ya waliopoteza maisha kufikia watu tisa, huku majeruhi wakibaki 16,” amesema Senyamule.
Ameongeza kuwa kati ya majeruhi 16, watu tisa wamepelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma ambako wanaendelea kupatiwa matibabu, huku wengine saba wakihudumiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chemba.
Senyamule ametoa pole kwa familia za marehemu na wote walioathirika na ajali hiyo, sambamba na kuwashukuru wananchi, viongozi wa wilaya, Jeshi la Polisi na wataalamu wa afya kwa msaada waliotoa katika shughuli za uokoaji na utoaji wa huduma kwa majeruhi.
“Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao na kuwaombea majeruhi wapone haraka. Pia nawashukuru wananchi, viongozi, Jeshi la Polisi na wahudumu wa afya kwa ushirikiano na msaada walioutoa kwa haraka,” amesema.
Taarifa zaidi kuhusiana na ajali hiyo zitaendelea kutolewa na mamlaka husika kadri uchunguzi unavyoendelea.

0 Comments:
Post a Comment