Mgombea wa Udiwani CCM Apotea Ghafla Sirari, Wananchi Wapaza Sauti

 


BAADHI ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sirari, wilayani Tarime mkoani Mara, wamelalamikia kupotea kwa mgombea wao wa udiwani, Geteba, aliyeshinda kura za maoni, wakimtaka Jeshi la Polisi kuingilia kati ili kubaini alipo.

Wananchi hao walijitokeza kwa wingi juzi katika uwanja wa wazi kwa ajili ya kumsindikiza mgombea wao kuchukua fomu ya kugombea udiwani, lakini walipata taarifa za kutokuwepo kwake baada ya kumsubiri kwa muda mrefu.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mara limethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea kufanyika ili kufahamu alipo.

Mkazi wa eneo hilo, Mwita Marwa, alisema:

“Sisi wakazi wa Kata ya Sirari tulijitokeza tangu saa sita mchana kwa ajili ya kumsindikiza mgombea wetu kuchukua fomu, lakini hadi saa 12 jioni tumenyeshewa mvua bila mafanikio. Tumepoteza muda mwingi na tumekasirishwa kwa sababu waliotuita walijua hayupo.”

Naye Bhoke Chacha, mkazi mwingine wa Sirari, alieleza kuguswa na tukio hilo kwa kusema:

“Kitendo hicho kimeumiza kwa sababu tulilazimika kuacha shughuli zetu, lakini hatukupata maelezo yoyote ya wazi kuhusu kutokuwepo kwake.”

Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tarime, Charles Temu, alisema:

“Ofisi yangu ilikuwa wazi muda wote. Wagombea walipaswa kufika kwa ajili ya kuchukua fomu na kufuata taratibu za tume, ikiwemo kula kiapo.”

Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamza Kyebanji, alithibitisha kupotea kwa mgombea huyo na kusema:

“Taarifa za kupotea kwa Geteba tayari zipo polisi. Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu alipo awasiliane na vyombo husika ili kuondoa sintofahamu.”

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, SACP Mark Njera, alionya dhidi ya kusambazwa kwa taarifa za uzushi, akisema:

“Jeshi linaendelea na uchunguzi. Tunawaomba wananchi wenye taarifa zitakazosaidia kumpata mgombea huyu wazipeleke mara moja kwa vyombo husika ili hatua stahiki zichukuliwe. Kueneza taarifa za uongo kuhusu watu kupotea ni kosa la jinai na linaweza kuleta taharuki kwa jamii.”

Tukio hili limezua maswali mengi miongoni mwa wanachama na wakazi wa Sirari, huku wengi wakitaka majibu ya haraka juu ya alipo mgombea huyo aliyekuwa tegemeo la wengi katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

0 Comments:

Post a Comment