MAJALIWA ATAKA MAGEREZA YOTE YAWE KWENYE NISHATI SAFI IFIKAPO 2027

 


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Nishati kushirikiana kuhakikisha kuwa magereza yote nchini yanaunganishwa na mifumo ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2027.



Akizungumza leo Jumamosi, Agosti 30, 2025, wakati wa uzinduzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika magereza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Majaliwa alisema hatua hiyo itaboresha huduma kwa wafungwa, kulinda afya za watumishi na kuhifadhi mazingira.



“Rais wetu Dkt. Samia anatambulika Afrika na duniani kwa ujumla kwa hamasa yake ya matumizi ya nishati safi, hatua hii mmeonesha kwa vitendo kwamba mnamuunga mkono,” alisema Majaliwa.

Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha gereza moja linaweza kutumia zaidi ya tani 100 za mkaa kwa mwaka zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 60, lakini kupitia matumizi ya nishati safi, gharama hizo zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50.

“Tafiti za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa moshi wa kuni na mkaa una kemikali hatarishi zinazoweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kama vile nimonia, kikohozi sugu na pumu,” alisema.

Aliwataka pia wawekezaji binafsi kuongeza ubunifu katika teknolojia za kupikia, huku akihimiza Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha wanatengeneza mazingira rafiki ya kisera na kodi kwa uwekezaji katika nishati safi.

“Pia kila taasisi, kila jamii na kila mwananchi ana jukumu katika matumizi ya nishati safi. Tuchukue hatua leo kwa manufaa ya kesho ya watoto wetu na vizazi vijavyo,” aliongeza.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo alisema mradi huo utasaidia sana katika utunzaji wa mazingira na kulinda afya za wapishi katika magereza.

“Jeshi letu la Magereza limefanikiwa kutekeleza kwa asilimia 100 matumizi ya nishati safi kwenye magereza,” alisema Sillo.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu alisema jeshi hilo limekuwa likitumia kuni kwa miongo mingi kwa ajili ya kupikia, ambapo kwa mwaka mahitaji yalikuwa ni wastani wa mita za ujazo 91,391.25.

“Hadi kufikia Desemba 2024, magereza yote nchini yalikuwa yameshaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya chakula cha wafungwa na mahabusu,” alisema.

“Mpaka sasa vyanzo vya nishati mbadala vinayotumika katika magereza ni gesi vunde (biogas), mkaa mbadala (briquettes), kuni poa na gesi asilia (natural gas).”

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali mstaafu Jacob Kingu alisema Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesaini mkataba wa shilingi bilioni 35.2 kwa ajili ya ruzuku ya kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa magereza yote nchini.

“Sisi REA tunatoa shilingi bilioni 26.5 sawa na asilimia 75.4, na Jeshi la Magereza linachangia shilingi bilioni 8.6 sawa na asilimia 24.6,” alisema.

Alisema fedha hizo zitatumika kujenga miundombinu 126 ya biogas na majiko banifu 377, ujenzi wa miundombinu 64 ya LPG na majiko banifu 256, usambazaji wa mitungi ya gesi 15,126 ya kilo 15, ununuzi wa mashine 61 za kutengenezea mkaa mbadala kwa kambi 22 za Magereza, pamoja na usambazaji wa makaa ya mawe tani 865 na majiko banifu 344.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Msimamizi wa Kitengo cha Kilimo, Mifugo na Utunzaji wa Mazingira kutoka Jeshi la Magereza, SACP Daimu Mmolosha alisema:

“Lengo la jeshi ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha nishati ili kuepuka utegemezi wa kuni na mkaa.”

0 Comments:

Post a Comment