CAG Kichere Afurahishwa na Uwekezaji Katika Makumbusho ya Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark



Na Mwandishi Wetu, Karatu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Charles Kichere, ametembelea Makumbusho ya Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark tarehe 29 Agosti 2025 na kupanda mti wa kumbukumbu katika eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kujifunza kuhusu urithi wa kijiolojia, kiutamaduni na kihistoria uliopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.



Katika ziara hiyo, Kichere aliambatana na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul-Razaq Badru pamoja na viongozi wengine wa menejimenti ya NCAA.



Akiwa ndani ya jengo hilo la makumbusho, Kichere alielezwa historia na umuhimu wa eneo hilo na Afisa Uhifadhi Mkuu, Dkt. Agnes Gidna, ambaye ni mtaalam wa urithi wa utamaduni kutoka NCAA. Baada ya maelezo hayo, CAG Kichere alionesha kufurahishwa na jitihada za uwekezaji zilizofanywa na NCAA.



"Nimevutiwa sana na namna ambavyo makumbusho haya yameandaliwa. Hii ni hazina kubwa kwa Taifa letu, sio tu kwa utalii bali pia kwa elimu na historia ya binadamu," amesema Charles Kichere.

Dkt. Agnes Gidna amesema:
"Makumbusho haya yamejengwa kwa lengo la kuhifadhi, kuelimisha na kuonesha urithi wa kipekee wa eneo la Ngorongoro Lengai UNESCO Geopark, ambalo lina historia ya aina yake duniani."


Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi, Abdul-Razaq Badru amesema:
"Tumewekeza kwenye makumbusho haya ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi na wageni kuhusu urithi wetu wa asili na historia. Tunataka wageni wakifika Ngorongoro, wasikie na waone historia na utamaduni wa eneo hili kwa kina."


Makumbusho hayo yamejengwa kwa kuzingatia vigezo vya UNESCO na yanatoa taswira pana ya Mlima Lengai — volkano hai ya kipekee duniani — pamoja na historia ya binadamu wa kale, jamii za wafugaji na vivutio vingine vya kipekee vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.


0 Comments:

Post a Comment