RC Kihongosi: Saluni Zizingatie Sheria, Usafi, Maadili – Marufuku Tozo ya Faini ya 30,000 Kufungua Maduka



Katika jitihada za kuboresha mazingira ya kazi na kukuza sekta ya huduma za urembo jijini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani  Kihongosi, amekutana na wamiliki na wafanyakazi wa saluni na vinyozi, ambapo ametoa maelekezo mbalimbali yenye lengo la kuboresha huduma, kuimarisha ajira, na kuondoa changamoto zinazokwamisha wafanyabiashara hao.

Mazingira ya Kazi na Ufuatiliaji wa Sheria



Akizungumza na mamia ya wafanyabiashara wa saluni na barbershop katika mkutano uliofanyika Julai 22, 2025, kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kihongosi aliwaeleza umuhimu wa kufuata sheria na taratibu za biashara ili waweze kuendesha shughuli zao bila bughudha kutoka kwa mamlaka za serikali.

 


“Tunataka kila mfanyabiashara awe mfano wa kuigwa katika kufuata sheria. Huu mkoa hauko hapa kuzuia watu kufanya kazi, bali kuwaunga mkono,” alisema Kihongosi.

Alibainisha kuwa saluni na barbershop ni maeneo muhimu ya ajira hasa kwa vijana, hivyo hayapaswi kugeuzwa sehemu za kukiuka maadili au kuendesha shughuli zisizofaa.



“Saluni zenu ni sehemu ya ajira kwa vijana wetu — tusizigeuze kuwa sehemu ya kuvunja maadili,” alisisitiza.


 

Aidha, aliwataka wamiliki wa biashara hizo kuhakikisha kuna usafi wa mazingira, matumizi salama ya vifaa, utoaji wa huduma bora kwa wateja, na kuzingatia taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni halali za biashara.

Changamoto Zaibuliwa na Wahusika

Wakati wa mkutano huo, wafanyabiashara walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo. Baadhi ya changamoto zilizojitokeza ni pamoja na:



  • Tozo na ushuru usioeleweka

  • Ukaguzi wa mara kwa mara usio na taarifa

  • Ukosefu wa mafunzo ya huduma bora na usalama kazini

  • Uhitaji wa mikataba ya ajira na elimu ya sheria

Marufuku Tozo ya Faini ya 30,000 Kufungua Maduka



Miongoni mwa masuala yaliyosisimua mjadala ni malalamiko kutoka kwa wamiliki wa saluni kuhusu kutozwa faini ya Shilingi 30,000 na baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Jiji la Arusha kama masharti ya kufunguliwa maduka yao baada ya kufungwa kwa kuchelewa kulipia leseni ya biashara au kodi ya huduma.

Kuhusu hilo, Kihongosi alitoa tamko rasmi la kupiga marufuku mara moja tozo hiyo ya faini ya "funguo", akisema ni kinyume cha sheria na ni unyanyasaji wa wafanyabiashara wadogo.

“Hii faini ya funguo haikubaliki. Sasa ukifunga saluni na kudai hela hizo kwa mwezi ni shilingi ngapi? Tutachukua hatua. Na naagiza Jiji la Arusha kuacha mara moja kufanya hivyo,” alisema Kihongosi kwa msisitizo.

Aliongeza kuwa tayari ameanza kuchunguza watumishi 11 wa idara ya biashara waliopo ndani ya Jiji la Arusha, na wale watakaobainika kuhusika katika kuchukua faini hizo watachukuliwa hatua za kisheria.

Mikopo Isiyo na Riba kwa Wafanyabiashara

Katika hatua ya kuwawezesha wajasiriamali kukuza mitaji yao, Kihongosi aliwataka wafanyabiashara hao kutumia fursa ya mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani.



Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, John Kayombo, alithibitisha uwepo wa shilingi bilioni 5.5 zilizotengwa kwa ajili ya mikopo hiyo, inayolenga wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu.



“Fedha hizi zipo. Zinapatikana bila riba. Tunawasihi wafanyabiashara wenye sifa wajitokeze kukopa ili kukuza mitaji yao,” alisema Kayombo.

Mafunzo na Ushirikiano wa Kudumu

Mkutano huo ulihitimishwa kwa makubaliano ya kuandaliwa kwa mafunzo maalum yatakayowasaidia wamiliki na wafanyakazi wa saluni na barbershop kuendesha biashara zao kwa tija na kwa kufuata sheria.

“Tutakuwa na vikao vya mara kwa mara na makundi haya. Lengo ni kuwajengea uwezo na kuhakikisha serikali iko bega kwa bega nao katika kutatua changamoto zao,” alisema Kihongosi.

Kwa upande wake, Hamimu Masoud, Meneja wa The New Sky Barbershop, alieleza kufurahishwa na ushirikiano huo mpya kati ya serikali na wafanyabiashara.

“Tumefurahi sana kwa mwaliko huu. Tumejifunza mengi, hasa namna ya kufuata sheria na kuwa sehemu ya maendeleo ya mkoa wetu,” alisema Masoud.

Kihongosi alihitimisha kwa kuwahimiza wafanyabiashara wa saluni kutoa taarifa kwa mamlaka wanapobaini matukio ya ukosefu wa amani au tabia zisizofaa kutoka kwa wateja au watendaji.

“Amani ya nchi ni tunu pekee. Tukiona dalili zozote zisizofaa, tuchukue hatua kwa kutoa taarifa mapema. Serikali iko tayari kushirikiana nanyi kwa kila hatua,” alisisitiza.

Mkutano huo umeacha taswira chanya kwa wajasiriamali wa huduma za urembo mkoani Arusha, huku matarajio yakiwa makubwa katika kuboresha mazingira ya biashara, huduma kwa wateja na ukuaji wa uchumi kupitia sekta ndogondogo.

0 Comments:

Post a Comment