OFISI YA MSAJILI WA HAZINA YALENGA KUKUSANYA SH2 TRILIONI

 

Kibaha, Pwani – Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeweka lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 2 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Shilingi bilioni 400 kutoka lengo la mwaka uliopita.


Hayo yalibainishwa Julai 28, 2025 na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, wakati wa uzinduzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yaliyoandaliwa na OMH kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi. Mafunzo hayo yamehusisha jumla ya watendaji wakuu 114 kutoka taasisi mbalimbali za umma, wakiwemo walioteuliwa hivi karibuni na wengine waliokuwa bado hawajapata mafunzo kama hayo licha ya kuwa kwenye nafasi kwa muda mrefu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mchechu alisema:
“Ili tuweze kufikia lengo letu la kukusanya Sh2 trilioni, itatubidi tuongeze bidii kwa asilimia 100 ya tulivyokuwa tunafanya mwaka wa fedha uliopita.”

Kwa mujibu wa taarifa za OMH, mwaka wa fedha uliopita (2024/25), ofisi hiyo ilifanikiwa kukusanya kiasi cha Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo ya kikodi, kiwango ambacho kilikuwa chini ya lengo la Sh1.6 trilioni lililowekwa na Serikali.

Mapato hayo yasiyo ya kikodi yanakusanywa kwa mujibu wa sheria mbalimbali za nchi na yanatokana na vyanzo kama gawio kutoka mashirika na taasisi za umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, na mapato ya ziada ya taasisi, pamoja na marejesho ya mikopo, riba, na makusanyo kupitia mfumo wa TTMS (Telecom Traffic Monitoring System).

Kwa mujibu wa Kifungu cha 180 cha Sheria ya Makampuni (Sura 212) na Kifungu cha 15(2)(b) cha Sheria ya Mashirika ya Umma (Sura 257), mashirika ya umma yanayofanya biashara yanawajibika kutoa gawio kwa Serikali. Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 12(3) cha Sheria ya Fedha za Umma Sura 348, taasisi za umma ambazo hazihusiki moja kwa moja na gawio zinatakiwa kuwasilisha asilimia 15 ya mapato ghafi kwa Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mchechu alisema:
“Tunaamini kuwa mafunzo haya yatakuwa chachu ya mageuzi katika mashirika ya umma, hasa kwa kuimarisha uongozi, maadili, uwajibikaji wa kifedha na usimamizi wa uwekezaji wa umma.”

Kufikia mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ilikuwa imewekeza takribani Sh86.25 trilioni katika taasisi za umma 252 na kampuni 56 ambazo Serikali ina hisa chache. Uwekezaji huu unahitaji usimamizi makini ili kuhakikisha unaongeza thamani kwa taifa na kuchangia kikamilifu katika mapato ya Serikali.

Kwa ujumla, jitihada za kuongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kikodi zinatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Serikali kupanua wigo wa mapato ya ndani bila kuongeza mzigo kwa walipa kodi wa kawaida.


0 Comments:

Post a Comment