Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (World Association of Press Councils – WAPC), huku pia akiteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (East Africa Press Councils – EAPC).
Uteuzi huo umefanyika wakati wa Mkutano wa Pili wa Mabaraza Huru ya Habari Barani Afrika (NIMCA) uliofanyika Julai 14–17, 2025, jijini Arusha, Tanzania.
Mkutano huo uliwakutanisha zaidi ya washiriki 500 kutoka mataifa mbalimbali, na uliratibiwa kwa mafanikio chini ya uongozi wa Sungura.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Yussuf Khamis Yussuf,
Kuchaguliwa kwake Sunguta kunatajwa kuwa ni ishara ya kuaminiwa kwa uongozi wake ndani ya tasnia ya habari barani Afrika na duniani. Akiwa Katibu Mkuu wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuiongoza WAPC, Sungura sasa ataiwakilisha Tanzania katika mijadala ya kimataifa kuhusu maadili, uhuru, na mustakabali wa uandishi wa habari.
Katika nafasi yake mpya, atashirikiana na David Omwoyo kutoka Kenya, ambaye amechaguliwa kuwa Rais wa WAPC na Mwenyekiti wa EAPC. Viongozi wengine walioteuliwa ni Peter Okello kutoka Uganda (Katibu wa EAPC), Habiba Alasow Mohamed kutoka Somalia (Mhazini wa EAPC), Ali Hancerli kutoka Cyprus ya Kaskazini (Makamu wa Kwanza wa Rais WAPC), Kishor Shrestha kutoka Nepal (Makamu wa Pili wa Rais WAPC), na Dkt. Tamer Ataburut kutoka Uturuki (Mhazini wa WAPC).
Kabla ya uteuzi huu, Sungura alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) kuanzia Mei 2024 hadi Julai 2025. Katika kipindi hicho, alijenga misingi imara ya uongozi na kuweka viwango vya kiutendaji kwa taasisi hiyo mpya. Uongozi wa NIMCA sasa umechukuliwa na Pathiswa Magopeni kutoka Afrika Kusini.

0 Comments:
Post a Comment