Mgombea urais wa Colombia, Miguel Uribe Turbay, mwenye umri wa miaka 39, yuko katika hali mahututi baada ya kupigwa risasi tatu, mbili kati ya hizo kichwani, wakati wa hafla ya kampeni iliyofanyika siku ya Jumamosi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bogotá.
Tukio hilo la kutisha lilitokea wakati Uribe alipokuwa akiwahutubia wafuasi wake katika bustani moja ya jiji hilo, kabla ya kushambuliwa kwa risasi na kijana anayeaminika kuwa na umri wa miaka 15, ambaye alikamatwa papo hapo na polisi, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Colombia.
Mke wa mgombea huyo, Maria Claudia Tarazona, amewaomba raia wote wa Colombia kusimama pamoja na familia yake katika kipindi hiki kigumu, huku akimtaka kila mmoja kumuombea mumewe apone.
“Miguel kwa sasa anapigania maisha yake, tumuombe Mungu aongoze mikono ya madaktari wanaomhudumia,” alisema Maria Claudia kwa huzuni mkubwa.
Chama cha Centro Democrático, ambacho Uribe anakuwakilisha katika mbio za kuwania urais, kimelaani vikali shambulio hilo na kukitaja kuwa kitendo cha kuvunja misingi ya uhuru na demokrasia nchini humo.
“Tunalaani vikali shambulio hili. Ni tishio kwa demokrasia na uhuru nchini Colombia,” ilisomeka taarifa rasmi ya chama hicho.
Hali ya mgombea huyo inaripotiwa kuwa tete, na madaktari wanaendelea kupambana kuokoa maisha yake katika hospitali moja ya Bogotá, ambapo amepelekwa kwa ajili ya matibabu ya dharura.
Tukio hili limeibua hisia kali miongoni mwa raia wa Colombia na viongozi wa kisiasa, huku wengi wakieleza hofu kuhusu usalama wa wagombea na mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.

0 Comments:
Post a Comment