Mapadri Watembelea Ngorongoro, Wahimiza Utunzaji wa Mazingira

 


Mapadri 11 kutoka parokia mbalimbali za Jimbo Katoliki la Singida, leo tarehe 18 Juni 2025, wamefanya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro kwa lengo la kujionea maajabu ya uumbaji wa Mungu na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira.



Padri John Makabe, kiongozi wa msafara huo, amesema ziara hiyo imelenga kuutambua uzuri wa kazi ya Mungu na kuongeza uelewa kwa watumishi wa kanisa kuhusu nafasi yao katika kulinda mazingira.

"Tumekuja kuona mazingira na kuhimiza utunzaji wake, neno la Mungu katika kitabu cha Mwanzo tumeambiwa Mungu aliumba vitu vyote na kuwakabidhi binadamu ili wavitunze na kuvilinda. Sisi watumishi wa Mungu ni sehemu ya utume wetu kuelezea habari ya umuhimu wa kutunza mazingira.



Ziara yetu hapa Ngorongoro imetusaidia kuona ukweli wa maajabu ya Mungu kupitia hifadhi hii. Tutaendelea kuhamasisha watu kutambua umuhimu wa mazingira kama zawadi tuliyopewa na Mungu ili tuyatunze, na yenyewe yatutunze kwa vizazi na vizazi," amesema Padri Makabe.



Wakati wa kuwapokea wageni hao, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia huduma za Utalii na Masoko, Mariam Kobelo, amesema kuwa Ngorongoro imeendelea kuwa kivutio muhimu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

"Jitihada za Serikali na wadau wa sekta binafsi kutangaza vivutio vya utalii nchini zimeendelea kuzaa matunda. Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro unahakikisha kuwa wageni wote wanapata huduma bora na kufurahia shughuli za utalii wanapokuwa ndani ya hifadhi," amesema Mariam Kobelo.

Ziara hiyo ni sehemu ya mwamko mpya kwa viongozi wa dini kuunga mkono juhudi za kitaifa katika kuhifadhi mazingira na kukuza utalii endelevu nchini.

0 Comments:

Post a Comment