Kesi ya uhaini inayomkabili, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Mahakama ya Tanzania imetangaza kuwa mwenendo wa kesi hiyo utarushwa mubashara kwa umma kupitia mitandao rasmi ya Mahakama hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mahakama ya Tanzania kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Gerard Julius Chami, lengo la kurusha mubashara kesi hiyo ni kuhakikisha uwazi na kutoa fursa kwa wananchi kufuatilia bila kufika mahakamani moja kwa moja.
"Lengo la Mahakama kurusha mubashara matangazo ya mwenendo wa mashauri haya ni kuwawezesha Wananchi popote pale walipo na ambao wanapenda kufuatilia mwenendo wa mashauri kuweza kufuatilia bila kuwa na ulazima wa kufika Mahakamani," alisema Chami.
Mahakama imeeleza kuwa chumba cha mahakama hiyo kina uwezo wa kuchukua watu 80 tu, hivyo nafasi za kuhudhuria zitatolewa kwa idadi maalum ya watu wakiwemo mawakili wa serikali, mawakili wa utetezi, waandishi wa habari na watu wachache walioteuliwa.
"Tunaomba Umma ufahamu kuwa, Mahakama ya Wazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam - Kisutu ni ndogo ikiwa na uwezo wa kuchukua watu 80 tu," alieleza Chami."Kwa uwezo huo imekubalika watakaoingia ni Mawakili wa Serikali na Watu wengine (10), Mawakili Utetezi na Watu wengine (60) na Waandishi wa Habari (10)," aliongeza.
Aidha, Mahakama imesema hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki.
Katika kesi hiyo ya Jinai Namba 8606/2025 na 8607/2025 kati ya Jamhuri dhidi ya Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na madai ya kutoa matamshi ya kuhamasisha mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini.
Wananchi wanaotaka kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo wametakiwa kujiunga na akaunti rasmi za Mahakama ya Tanzania katika mitandao ya kijamii au kutembelea tovuti yao rasmi www.judiciary.go.tz ambapo kiungo cha matangazo hayo kitapatikana kabla ya saa 2:30 asubuhi.
Aidha, kwa wale watakaohudhuria mahakamani, wametakiwa kufuata miongozo yote ya kiafya kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Afya kupitia taarifa iliyotolewa tarehe 20 Mei, 2025.
"Mahakama inawahakikishia umma na Watanzania wote kuwa itaendelea kutoa haki kwa uwazi, kwa wakati na kwa wote. Tunawahimiza Wananchi wote kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kujenga mfumo wa utoaji haki unaozingatia misingi ya Kikatiba, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali," alisisitiza Chami.



0 Comments:
Post a Comment