Gawio la Kihistoria: Mageuzi ya Taasisi za Umma Yaanza Kuzaa Matunda

 


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kiasi cha Sh1.028 trilioni kama gawio na michango mingine kutoka kwa mashirika ya umma na kampuni ambazo ina hisa, ikiwa ni mafanikio makubwa ya utekelezaji wa mageuzi madhubuti yaliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.



Takwimu hizo zimebainishwa katika hafla maalum ya "Gawio Day", ambapo mafanikio haya yametajwa kuwa ni matokeo ya maelekezo ya ufanisi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa taasisi za umma, sambamba na mikakati ya kuongeza tija iliyowekwa tangu kuanza kwa uongozi wake.



Akizungumza katika tukio hilo, Rais Samia alieleza kuwa ongezeko hilo la mapato ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya mashirika ya umma, mabadiliko yanayolenga kujenga taasisi imara, zenye uwezo wa kujitegemea na kuchangia kikamilifu maendeleo ya Taifa.

“Nimefurahishwa sana na ongezeko hili la mapato lisilo na mfano tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina mwaka 1959. Hii ni hatua kubwa katika safari yetu ya mageuzi,” alisema.

Aidha, Rais alibainisha kuwa Serikali bado ina malengo makubwa zaidi kwa mwaka ujao wa fedha, likiwemo lengo la kuvuka kiwango cha Sh1.5 trilioni, hatua itakayowezesha mashirika kuwa na mchango wa moja kwa moja katika uchumi wa Taifa.



Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na utekelezaji wa falsafa ya "R4", hasa kipengele cha "Reforms and Rebuild", sambamba na usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa utendaji wa taasisi.

Katika kuendeleza kasi ya mageuzi, Rais alitoa maagizo manne muhimu kwa taasisi hizo:

  1. Ubunifu katika kutatua changamoto na kuongeza tija;

  2. Kukamilisha Sheria ya Uwekezaji wa Umma kwa haraka ili kuweka misingi imara ya uwekezaji;

  3. Kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, ufanisi na ufuatiliaji wa matumizi;

  4. Kuwajengea uwezo watumishi wa taasisi na kuwapa motisha stahiki kwa ajili ya kuongeza ari ya kazi.

"Ni muhimu taasisi zetu zionyeshe ubunifu na kutafuta njia mbadala za kuboresha utendaji badala ya kusubiri kila suluhisho kutoka Serikali Kuu," alisisitiza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Msajili wa Hazina, taasisi 213 zimeshiriki katika utoaji wa gawio hilo, likiwa ni ongezeko la asilimia 68 ikilinganishwa na mwaka uliopita — hatua inayodhihirisha ukuaji wa uwajibikaji wa mashirika na mchango wao katika kuimarisha uchumi wa Taifa.

Mafanikio haya ni kiashirio cha mwelekeo mpya wa uendeshaji wa taasisi za umma nchini Tanzania, ambapo uwazi, ufanisi na ubunifu vinawekwa mbele kama misingi ya maendeleo endelevu.



0 Comments:

Post a Comment