DIRISHA LA MAOMBI YA MIKOPO YA ELIMU KUFUNGULIWA JUNI 15, 2025

 


Serikali imetangaza kuwa miongozo ya mikopo ya elimu kwa mwaka wa masomo 2025/2026 sasa itapatikana katika lugha za Kiswahili na Kiingereza kupitia tovuti za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz) pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (www.heslb.go.tz).

Tangazo hilo limetolewa leo Juni 6, 2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, ambapo alieleza kuwa dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao litafunguliwa kuanzia Juni 15 hadi Agosti 31, 2025.

"Waombaji wanatakiwa kuisoma miongozo hiyo kwa siku kumi kabla ya kuanza mchakato wa kuomba ili kuelewa vigezo na masharti ya utoaji mikopo," amesema Prof. Nombo.

Aidha, ameeleza kuwa mwaka huu waombaji hawatalazimika kutuma nakala ngumu za maombi kama ilivyokuwa kwa mwaka wa 2024/2025, kutokana na maboresho yaliyofanyika kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

"Maboresho haya yamelenga kurahisisha mchakato wa utoaji mikopo na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wanafunzi wanaostahili," amesema.

Katika miongozo hiyo, imesisitizwa kuwa kila mwombaji anatakiwa kuwa na akaunti ya benki kwa ajili ya malipo ya moja kwa moja chuoni, pamoja na namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake ili kupokea ujumbe muhimu kutoka Bodi ya Mikopo.

Kuhusu ruzuku ya Samia Scholarship, Profesa Nombo amesema, "Tarehe ya kufungua dirisha la maombi ya Samia Scholarship itatangazwa baada ya NECTA kutangaza matokeo ya kidato cha sita mwaka 2025."

Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kurahisisha taratibu za utoaji wa mikopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaostahili wanapata huduma kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Miongozo hiyo inatarajiwa kuwa nyenzo muhimu kwa waombaji katika kuelewa namna bora ya kuwasilisha maombi yao kwa mafanikio.


0 Comments:

Post a Comment