Aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, Afariki Dunia Akiwa na Umri wa Miaka 68

 



Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Chagwa Lungu, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, chama chake cha Patriotic Front (PF) kimethibitisha. Lungu alifariki mapema Alhamisi asubuhi katika kituo cha tiba maalum kilichopo Pretoria, Afrika Kusini, ambako alikuwa akipokea matibabu ya hali ya kiafya iliyomsumbua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya PF iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii, Lungu alikuwa akihudumiwa kwa uangalizi maalum katika wiki za hivi karibuni kabla ya kufariki dunia. Taarifa hiyo pia ilijumuisha video ya binti yake, Tasila Lungu, ambaye pia ni Mbunge wa Zambia, akitangaza kifo cha baba yake.

“Baba yangu alikuwa chini ya uangalizi wa kitabibu kwa wiki kadhaa zilizopita. Hali yake ilikuwa ikisimamiwa kwa heshima na faragha,” alisema Tasila.

Edgar Lungu, aliyekuwa Rais wa sita wa Zambia, aliongoza taifa hilo la Kusini mwa Afrika kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, kabla ya kushindwa katika uchaguzi na mpinzani wake wa muda mrefu, Hakainde Hichilema, ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Zambia.

Lungu alichukua madaraka baada ya kifo cha mtangulizi wake, Michael Sata, mwaka 2015. Kabla ya hapo, alihudumu kama Waziri wa Sheria na Waziri wa Ulinzi.

Akiwa madarakani, Lungu alipata sifa kwa kusimamia mpango mkubwa wa ujenzi wa barabara, lakini pia alikosolewa vikali kwa kuisukuma Zambia kwenye mzigo mkubwa wa madeni ya kimataifa. Taifa hilo liliacha kulipa madeni yake mwaka 2020, jambo lililoathiri sana nafasi yake ya kushinda uchaguzi wa 2021.

“Urithi wa Edgar Lungu ni wa aina mbili. Ataendelea kukumbukwa kwa kuvumilia vitendo vya kihuni kutoka kwa wafuasi wake, lakini pia alikuwa ni aina ya mwanasiasa aliyeweza kuwasogelea wananchi wa tabaka la chini,” alisema mchambuzi wa siasa Lee Habasonda kutoka Chuo Kikuu cha Zambia.

“Aliruhusu hata masikini kabisa wa Zambia kusogea karibu na kumbi za mamlaka, jambo ambalo halikuwa la kawaida katika siasa za nchi hii,” aliongeza Habasonda.

Mara tu baada ya kuingia madarakani mwaka 2015, Lungu alifanya mabadiliko kadhaa ya kisheria yaliyotajwa kuwa ya maendeleo, ikiwemo kurekebisha katiba na kupunguza mamlaka ya Rais. Hata hivyo, alikuja kujaribu kufuta baadhi ya marekebisho hayo baadaye bila mafanikio.

Katika miaka yake ya mwisho madarakani, Lungu alikosolewa kwa kushindwa kuwajibisha wafuasi wake waliodaiwa kuhusika na vitendo vya fujo na ukatili wa kisiasa.

Baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2021, Lungu alistaafu siasa, lakini alirejea tena mwaka 2023 na kuchaguliwa kuwa kiongozi na mgombea urais wa muungano wa vyama vya upinzani ulioongozwa na Patriotic Front. Hata hivyo, Disemba 2024, Mahakama ya Katiba ya Zambia ilitoa uamuzi kwamba hastahili tena kugombea urais.

Edgar Lungu alizaliwa Novemba 11, 1956, katika mji wa Ndola, eneo la copperbelt, na alikuwa mwanasheria kwa taaluma. Katika maisha yake ya kisiasa, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri kabla ya kuwa Rais.

Katika maisha yake binafsi, alijieleza kama “Mzambia wa kawaida aliyetoka katika maisha ya kawaida kabisa.”

Kifo chake kinakuja miezi sita baada ya ndoto yake ya kurejea madarakani kuhitimishwa rasmi na mahakama, na kimeacha pengo kubwa katika siasa za Zambia, hasa miongoni mwa wafuasi wake wa PF.

Rais Hakainde Hichilema na viongozi wengine wa kitaifa wanatarajiwa kutoa salamu za rambirambi rasmi wakati taifa hilo linaanza maandalizi ya maziko ya mmoja wa marais wake waliopita.

0 Comments:

Post a Comment