Waliokuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa hadi Januari 22, 2025, wametangaza rasmi kujiondoa katika chama hicho wakieleza sababu mbalimbali ikiwemo kutokuheshimiwa kwa katiba ya chama, ubaguzi wa wanachama na kukosekana kwa utaratibu wa kufanya maamuzi kwa njia ya vikao halali.
Viongozi hao ni Benson Kigaila (aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Bara), Salum Mwalimu (aliyekuwa Katibu Mkuu CHADEMA Zanzibar), aliyekuwa Katibu Mkuu BAWACHA, Catherine Ruge, na Waliokuwa Wakurugenzi Julius Mwita na John Mrema.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake katika mkutano na wanahabari uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Kigaila alisema:
"Sisi tumeamua wote kwa pamoja tunajiondoa CHADEMA ili tuwaachie hicho chama waendeshe wanavyotaka. Hatutaki kuwa wanachama wa chama ambacho maamuzi hayafanywi kwa vikao, ambacho wanachama wanabaguliwa na katiba haifuatwi. Sisi siyo chawa, sisi ni viongozi tunajitambua."
Kigaila aliweka wazi kuwa walijiunga CHADEMA kwa malengo ya kisiasa na kwamba sasa chama hicho kimepoteza mwelekeo wa malengo hayo.
"Tuliingia CHADEMA kwa malengo na tunatoka CHADEMA kwa sababu malengo hayo yamepotea. Tunawaachia chama chao."
Kuhusu mustakabali wao wa kisiasa, Kigaila alisema:
"Nisije nikaachiwa maswali, mtu aseme sasa tunaenda wapi? Sisi sio wazee waliokata tamaa wala waliostaafu siasa. Tutaendelea kuwapigania Watanzania, na tutatafuta jukwaa muafaka ambalo tutalifanya kazi hiyo."
Aidha, Kigaila alifichua hali ya sintofahamu ndani ya chama kwa kusema kuwa:
"Siku hizi kwenye chama kila mtu anayejulikana kuwa alimuunga mkono Freeman Mbowe kwenye uchaguzi wa mwenyekiti anaitwa msaliti. Sasa sisi tunajiuliza, hivi kumuunga mkono Mbowe, ambaye alikuwa mwenyekiti halali wa CHADEMA, iweje sasa iwe usaliti?"
Aliongeza kuwa alishauriana na Katibu Mkuu wa sasa wa CHADEMA mnamo Januari 24, 2025, kuhusu haja ya kuimarisha umoja ndani ya chama, lakini ushauri huo haukufanyiwa kazi.
"Nilimshauri arejeshe umoja kwa sababu safari yetu ni ndefu na ngumu, inahitaji mshikamano. Nilisema kaulimbiu ya mkutano mkuu ilikuwa 'Stronger Together', lakini hali ya sasa ni ya kugawanyika, watu wanabaguliwa, wanatishwa na kukandamizwa."
Katika hatua nyingine, Kigaila alieleza kusikitishwa na namna Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu, alivyomshambulia hadharani Freeman Mbowe baada ya uchaguzi.
"Baada ya Mbowe kuzungumza kwa busara na kutoa ushauri wa kuunda Tume ya Maridhiano, Tundu Lissu alisimama na kuendelea kumshambulia. Hilo lilituma ujumbe kuwa kampeni bado zinaendelea hata baada ya uchaguzi, na tangu siku hiyo, ubaguzi dhidi ya waliomuunga mkono Mbowe umeongezeka."
Mkutano huo wa kihistoria umeweka wazi mgawanyiko mkubwa ndani ya CHADEMA, huku viongozi hao wakiahidi kuendelea na harakati zao za kisiasa nje ya chama hicho.
"CCM siyo chaguo letu, lakini tutashauriana na vyama mbalimbali na tutaeleza tutakapoelekea. Kazi ya kuwatumikia Watanzania haijakamilika," alihitimisha Kigaila.
Hatua hii inatafsiriwa na wachambuzi wa siasa kama pigo kwa CHADEMA huku ikiashiria kuibuka kwa harakati mpya za kisiasa kutoka kwa viongozi waliokuwa wakiheshimika ndani ya chama hicho.

0 Comments:
Post a Comment