KIFO CHA MZEE CLEOPA DAVID MSUYA: TAIFA LAPOTEZA NGUZO YA UONGOZI NA HEKIMA
IJUE HISTORIA YAKE
Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Cleopa David Msuya, amefariki dunia leo, Jumatano tarehe 7 Mei 2025, katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Mzee Msuya, aliyekuwa akipatiwa matibabu ya matatizo ya moyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 94.
Akithibitisha taarifa hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kuanzia leo hadi Mei 13, 2025. Katika kipindi hicho, bendera zote za taifa zitapepea nusu mlingoti.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema: “Kwa masikitiko makubwa, napenda kuwajulisha Watanzania wote kuhusu msiba wa kitaifa wa kifo cha mzee wetu, Mhe. Cleopa David Msuya. Taifa limepoteza mtu muhimu sana katika historia ya uongozi wa nchi yetu.” Aliongeza kuwa, “Taarifa zaidi kuhusu msiba huu zitaendelea kutolewa na Serikali. Nawapa pole sana Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa.”
WASIFU NA MCHANGO WAKE KATIKA TAIFA
Mzee Cleopa David Msuya alizaliwa tarehe 4 Novemba 1931 mkoani Kilimanjaro. Alianza kazi ya utumishi wa umma akiwa kijana na baadaye kuingia katika uongozi wa juu wa serikali kwa nyadhifa mbalimbali.
Mwaka 1980, aliteuliwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, akichukua nafasi ya Edward Moringe Sokoine aliyekuwa masomoni Ulaya wakati huo. Alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 1983, alipoachia kijiti kwa Sokoine baada ya kurejea nchini.
Kwa mara ya pili, aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu na Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, mnamo Desemba 1994, akichukua nafasi ya John Samuel Malecela. Alidumu kwenye wadhifa huo hadi Novemba 1995, alipomkabidhi madaraka Frederick Sumaye.
Mbali na Uwaziri Mkuu, Msuya aliwahi kushika nafasi nyingine nyeti kama Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara, pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, Mzee Msuya alijitosa katika kinyang'anyiro cha kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, hakufanikiwa kushinda mchujo ndani ya chama baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Jakaya Mrisho Kikwete na Benjamin William Mkapa, ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
MCHANGO WAKE NA URITHI WA KITAIFA
Mzee Msuya atakumbukwa kwa maadili ya hali ya juu, busara, na msimamo wa kizalendo katika utumishi wake wa umma. Alikuwa miongoni mwa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika kujenga misingi ya uchumi wa taifa, hasa akiwa Waziri wa Fedha katika vipindi vya mpito vya kihistoria.
Katika salamu zake za pole, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema: “Mzee Msuya alikuwa kiongozi aliyeamini katika mazungumzo, mshikamano, na uzalendo wa kweli. Tumepoteza hazina kubwa ya hekima.”
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Dkt , Emmanue Nchimbi alitoa salamu za pole akisema: “Alikuwa nguzo ya CCM, muumini wa haki na usawa, na mfano wa kuigwa kwa viongozi wa kizazi kipya.”
MAANDALIZI YA MAZISHI
Serikali imeeleza kuwa mipango ya mazishi ya kitaifa inaandaliwa na taarifa rasmi kuhusu tarehe na sehemu ya mazishi itatangazwa baadaye. Viongozi wa kitaifa, mashirika ya kijamii, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameanza kumiminika kutoa rambirambi kwa familia ya marehemu.
Mzee Cleopa David Msuya ataendelea kukumbukwa kama kiongozi aliyelitumikia taifa kwa moyo wa dhati na kwa zaidi ya miongo minne ya utumishi wa umma.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Cleopa David Msuya mahali pema peponi. Amina.




0 Comments:
Post a Comment