Rais wa Ufaransa Apigwa Kibao na Mkewe? Video Yazua Gumzo Mitandaoni, Élysée Yatoa Ufafanuzi

 


Ziara ya kitaifa ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, nchini Vietnam imevuta hisia za kimataifa kufuatia video inayomuonesha akipokea kile kilichoelezwa na baadhi ya wachambuzi wa mitandaoni kama “kibao cha uso” kutoka kwa mke wake, Brigitte Macron.

Katika video hiyo iliyorushwa na televisheni ya Reuters, mkono wa Brigitte – ambao ndiyo sehemu pekee ya mwili wake iliyokuwa ikionekana – unagusa uso wa Macron akiwa nje ya ndege ya rais, punde tu baada ya kuwasili Hanoi. Rais Macron anaonekana kugeuka na kumtazama mkewe, kisha anaangalia kamera na kuwapungia mkono waliokusanyika kumpokea.

Tukio hilo liliibua uvumi mwingi katika mitandao ya kijamii, huku wengine wakidai Brigitte alimpiga mumewe. Hata hivyo, watu wa karibu na wanandoa hao walikanusha madai hayo, wakisisitiza kuwa kilichotokea ni masihala ya kawaida ya kifamilia kabla ya shughuli rasmi kuanza.

“Ilikuwa ni wakati wa kupumzika kidogo na kufurahia kabla ya shughuli rasmi kuanza,” chanzo kimoja kililiambia shirika la habari la dpa.

Mmoja wa washauri wa rais huyo alieleza kuwa tukio hilo lilichukuliwa vibaya kimakusudi na wale “wanaotafuta kila fursa ya kuchafua jina la Macron.”

“Hilo tu liliwatosha waumini wa nadharia za njama kupata jambo la kulizungumzia,” alieleza.

Urusi na Nadharia za Njama

Kwa mujibu wa duru kutoka Ufaransa, televisheni ya serikali ya Urusi, RT (Russia Today), hapo awali imeshawahi kueneza tuhuma kuwa Rais Macron hupigwa na mkewe – madai ambayo sasa yamechukua sura mpya kupitia video hiyo.

“Madai kama haya ni ya kudhalilisha na yanaendeshwa na mitandao ya upotoshaji wa kidijitali inayolenga kuchafua viongozi wa mataifa ya Magharibi,” alisema afisa mmoja wa serikali ya Ufaransa aliyeomba hifadhi ya jina.

Mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya yamefuta leseni ya kurusha matangazo ya RT kwa madai ya kueneza propaganda na taarifa za uongo, hasa zinazohusiana na vita vya Ukraine na siasa za Ulaya.

Tuhuma Nyingine: Kokaini Safarini Kiev

Katika tukio jingine, Ikulu ya Élysée ilikanusha ripoti ya uongo kuhusu kifurushi kilichodaiwa kuwa na dawa za kulevya aina ya kokaini, kilichosemekana kuwa mali ya Macron wakati wa safari yake ya treni kwenda Kiev. Tovuti iliyoeneza taarifa hiyo imetajwa kuwa sehemu ya mtandao wa upotoshaji unaoendeshwa na Urusi.

“Taarifa hizo ni za kutungwa na hazina msingi wowote. Rais Macron ameendelea kuwa mhimili wa kupambana na siasa za hadaa barani Ulaya,” alisema msemaji wa Élysée.

Ziara Inaendelea Licha ya Uvumi

Licha ya minong’ono hiyo, Rais Macron na mkewe wanaendelea na ziara yao katika nchi za Vietnam, Indonesia, na Singapore. Ziara hiyo inalenga kujadili masuala ya ulinzi wa kikanda, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, na fursa za kiuchumi kati ya Ufaransa na mataifa hayo ya Kusini-Mashariki mwa Asia.

Katika ujumbe wake kwa waandishi wa habari mjini Hanoi, Macron alisema:

“Uhusiano kati ya Ufaransa na Asia ya Kusini ni muhimu kwa amani, maendeleo endelevu, na mwelekeo mpya wa kijamii na kiuchumi.”

Ziara hiyo inatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa. Matarajio ya Ufaransa ni kuimarisha ushawishi wake wa kiuchumi na kisiasa katika eneo linalokua kwa kasi zaidi duniani kiuchumi.


0 Comments:

Post a Comment