RAIS SAMIA ATUNUKIWA MEDALI YA HESHIMA KUTOKA UAE

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Medali ya heshima ya Mother of the Nation Order kutoka kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan.



Medali hiyo iliwasilishwa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 5 Mei 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, Sheikh Abdullah Bin Zayed Al Nahyan.

Kwa mujibu wa taarifa, medali hiyo ni moja ya medali za juu kabisa zinazotolewa na UAE na hutolewa kutambua mchango wa viongozi wanaoleta maendeleo endelevu kwa jamii zao.

Serikali ya UAE imetambua juhudi za Rais Samia katika kuwaletea Watanzania maendeleo yanayochochea ustawi wa kijamii, uwezeshaji wa wanawake, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Sheikh Abdullah alitoa salamu kutoka kwa Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan akisema: "Tunatambua juhudi kubwa za Rais Samia katika kuimarisha maendeleo endelevu, usawa wa kijinsia na mshikamano wa kimataifa. Tunawatakia Watanzania kheri na mafanikio zaidi."

Aidha, Sheikh Abdullah alisisitiza dhamira ya UAE kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili: "Tutaendelea kupanua ushirikiano wetu katika sekta muhimu kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili."

Tanzania na UAE zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu unaojengwa katika misingi ya heshima, ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya pamoja.


0 Comments:

Post a Comment