Katika kile kinachoonekana kuwa ni mvutano mpya wa kidiplomasia kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania, Bunge la Ulaya limejadili na kupitisha maazimio yenye uzito kuhusu hali ya kisiasa na haki za binadamu nchini Tanzania, huku likimpa uzito mkubwa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, aliyekamatwa hivi karibuni.
Maazimio hayo yamepokelewa kwa hasira na kupingwa vikali na Bunge la Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maazimio ya Bunge la Ulaya
Katika kikao cha dharura kilichofanyika mjini Brussels, wabunge wa Bunge la Ulaya walijadili na kutoa maazimio kadhaa wakieleza wasiwasi wao juu ya kile walichokitaja kuwa ni kuzorota kwa hali ya haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari, na ukandamizaji wa kisiasa nchini Tanzania. Maazimio hayo yamejikita katika masuala yafuatayo:
-
Kumwachilia Huru Tundu Lissu: Wabunge hao wameitaka Serikali ya Tanzania kumwachilia mara moja na bila masharti yoyote Tundu Lissu, wakidai kuwa mashtaka dhidi yake yanaonekana kuwa ya kisiasa na yenye kuhusisha hatari ya maisha. Pia wametaka apewe haki ya kusikilizwa kwa haki, upatikanaji wa msaada wa kisheria, na kulindwa usalama wake.
-
Kukomesha Ukandamizaji wa Kisiasa na Kijamii: Bunge hilo limeitaka Serikali ya Tanzania kusitisha mara moja ukamataji holela, mashambulizi, unyanyasaji, na vitisho dhidi ya wanasiasa wa upinzani, watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa LGBTIQ+, waandishi wa habari, watu wa kiasili na mashirika ya kiraia. Pia wametaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu dhuluma za polisi na watu waliopotea.
-
Marekebisho ya Kisheria: Wametaka sheria za uhalifu wa mtandaoni na zile zinazohusu vyombo vya habari zirekebishwe ili ziendane na sheria za kimataifa za haki za binadamu, na kutoa wito kwa uhuru wa kujieleza, uhuru wa mahakama, na wa vyombo vya habari kuheshimiwa.
-
Uchaguzi Huru 2025: Wabunge hao wamehimiza ushiriki kamili wa Chadema na vyama vingine vya siasa katika uchaguzi wa Oktoba 2025, huku wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo jumuishi kuhusu mageuzi ya uchaguzi kwa kushirikiana na mashirika ya kiraia na wadau wa ndani.
-
Kufuatilia Kesi ya Lissu: EU na nchi wanachama wake wametakiwa kuwasiliana kwa kina na mamlaka za Tanzania kuhusu kesi ya Lissu na kufuatilia kwa karibu mwenendo wake. Imetolewa tahadhari kuwa endapo hali ya haki za binadamu itaendelea kuzorota, hatua stahiki zichukuliwe.
-
Kufuta Hukumu ya Kifo: Bunge hilo limeitaka Tanzania ifute rasmi adhabu ya kifo na kubadilisha hukumu zote zilizotolewa kwa msingi huo.
-
Mshikamano wa Misaada na Haki za Binadamu: Wamekumbusha kuwa misaada ya maendeleo kutoka EU, ikiwemo mpango wa Global Gateway, inapaswa kulingana na uendelezaji wa haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata haki.
-
Uwasilishaji wa Azimio: Rais wa Bunge la Ulaya ameagizwa kupeleka rasmi azimio hilo kwa Serikali ya Tanzania, Bunge la Taifa, na Umoja wa Afrika.
Bunge la Tanzania Lapinga Maazimio
Saa chache baada ya kuibuka kwa taarifa hizo, Bunge la Tanzania lilikutana mjini Dodoma na kupinga kwa sauti kubwa baadhi ya vipengele vya maazimio hayo, hususan lile linalohusiana na haki za watu wa mapenzi ya jinsia moja.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, alikosoa vikali azimio la pili la Bunge la Ulaya linalohimiza kutambuliwa kwa haki za watu wa LGBTIQ+, akilitaja kuwa "ni dharau kwa Mungu, kwa Taifa na kwa misingi ya kijamii ya Watanzania."
"Yalitolewa maazimio 6 kwa ajili ya Serikali ya Tanzania, na moja ya azimio ni kuhusu Tundu Lissu, hiyo sina shida nayo kesi iko mahakamani, lakini lipo azimio namba mbili la kutambua haki ya mapenzi ya jinsia moja," alisema Chiwelesa.
Msimamo wa Serikali ya Tanzania
Kupitia tamko rasmi, Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa hatua zote za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya raia au viongozi wa kisiasa zinafuata misingi ya sheria na utawala wa haki. Serikali imeeleza kutoshawishika na mashinikizo ya nje, hasa yale yanayopingana na misingi ya kijamii, kiutamaduni na kiimani ya nchi.
Maazimio haya yamefungua ukurasa mpya wa mjadala wa kimataifa kuhusu hali ya demokrasia, haki za binadamu na uhuru wa kisiasa nchini Tanzania.
Iwapo yatapitishwa na Bunge la Ulaya, hatua hizo huenda zikawa na athari za muda mrefu katika ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya.
Hali inayoendelea kufuatiliwa kwa karibu na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Je, Tanzania itachukua hatua za kurekebisha mwenendo wake wa kisiasa, au itaendelea kupinga shinikizo la kimataifa kwa misingi ya uhuru wa kitaifa? Muda ndio utakaoamua.

0 Comments:
Post a Comment