Katika tukio la kihistoria kwa taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),Huenda RC aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, akawa mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, uhalifu wa kivita, na kushirikiana na makundi ya waasi. Hatua hii imechukuliwa baada ya Bunge la Seneti kuondoa kinga yake ya kisheria kama seneta wa maisha, na hivyo kufungua njia ya kufunguliwa mashtaka rasmi.
Katika kikao maalum kilichofanyika jijini Kinshasa, jumla ya maseneta 88 walipiga kura kuunga mkono kuondolewa kwa kinga hiyo, huku watano pekee wakipinga, na kura tatu zikibatilishwa. Kabila, ambaye hajaonekana hadharani tangu aondoke nchini mwaka 2023, hakuhudhuria kikao hicho wala kutuma mwakilishi wake kwa ajili ya kujitetea.
“Huu ni wakati wa haki kushika hatamu. Hatuwezi kuendelea kuwa taifa la kusamehe uhalifu mkubwa unaogharimu maisha ya maelfu ya raia,” alisema Seneta Adolphe Onusumba, mmoja wa walioongoza hoja ya kuondolewa kwa kinga hiyo.
TUHUMA NZITO
Kabila anatuhumiwa kuhusika moja kwa moja na uungaji mkono wa kijeshi na kifedha kwa kundi la waasi la M23, ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi ya mara kwa mara mashariki mwa Congo, likiteka miji muhimu kama Rutshuru, Bunagana, na Goma mapema mwaka huu.
Tuhuma hizo pia zinamhusisha na kushiriki katika kupanga mashambulizi dhidi ya raia, pamoja na kukiuka mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Makundi ya kutetea haki za binadamu ndani na nje ya DRC yamekuwa yakitoa wito kwa miaka mingi wa kuwawajibisha viongozi waliotuhumiwa kushiriki au kufumbia macho uhalifu unaoendelea katika maeneo ya mashariki.
“Kumfungulia mashtaka Kabila ni ujumbe kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Wananchi wa Congo wanastahili kupata haki,” alisema Marie-Noëlle Mbala, mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Goma.
HISTORIA YA MGOGORO WA MASHARIKI MWA DRC
Mgogoro wa mashariki mwa Congo una mizizi mirefu inayochangiwa na mivutano ya kikabila, udhibiti wa rasilimali, na uingiliaji wa mataifa ya jirani. Tangu miaka ya 1990, makundi ya waasi zaidi ya 100 yamekuwa yakipigana kudhibiti maeneo tajiri kwa madini kama vile kobalti, dhahabu, na almasi. Serikali ya DRC kwa muda mrefu imeshindwa kudhibiti kikamilifu maeneo haya.
Kundi la M23, ambalo linatajwa kuungwa mkono na baadhi ya maafisa wa zamani wa serikali, lilianzishwa upya mwaka 2022 na limekuwa likitekeleza mashambulizi ya ghafla yaliyopelekea maelfu ya watu kukimbia makazi yao. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti visa vya mauaji, ubakaji wa wanawake na wasichana, na utekaji wa watoto kwa ajili ya kujiunga na jeshi la waasi.
“Tulilalamika kwa miaka mingi kuhusu ushiriki wa viongozi wakuu katika kuunga mkono makundi haya. Sasa tuna matumaini kuwa hatua hii italeta mabadiliko,” alisema Jean-Baptiste Katembo, mtafiti wa masuala ya amani kutoka Kivu Kusini.
HATUA INAYOFUATA
Baada ya kuondolewa kwa kinga ya kisheria, kesi dhidi ya Kabila sasa inatarajiwa kuwasilishwa rasmi katika mahakama ya juu ya DRC au kupitia mfumo wa mahakama za kimataifa ikiwa serikali ya Kinshasa itaamua kushirikiana na taasisi za haki za kimataifa.
Wachambuzi wa kisiasa wanaitazama hatua hii kama ishara ya mwanzo wa zama mpya za uwajibikaji barani Afrika, ambapo viongozi wa zamani wanahesabiwa kwa matendo yao wanapokuwa madarakani.
“Hili ni somo kwa viongozi wote Afrika. Kuna mwisho wa kila utawala, na historia huwa haifutiki,” alisema Prof. Didier Lukusa, mhadhiri wa siasa za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kinshasa.
Huku dunia ikifuatilia kwa karibu, macho sasa yanageukia serikali ya Rais Félix Tshisekedi kuona iwapo itaendeleza mchakato huu kwa haki, uwazi, na kwa kuzingatia misingi ya sheria.

0 Comments:
Post a Comment