Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche, ametangaza kuitishwa kwa kikao maalum cha Kamati Kuu ya chama hicho kitakachofanyika Juni 3, 2025 kwa ajili ya kujadili barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na kutoa mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho na taifa kwa ujumla.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi katika uzinduzi wa Operesheni ya "No Reforms, No Election" uliofanyika kwenye viwanja vya Soko Kuu jijini Arusha, Heche alisema hatua hiyo imekuja kufuatia msimamo wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kutotambua uongozi wa Chadema na kusitisha ruzuku ya chama hicho.
“Tumeitisha Kamati Kuu ya chama tarehe 3 Juni, kujadili barua ya Msajili na baada ya hapo tutatoa mwelekeo wa taifa ni wapi tunaelekea,” alisema Heche huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
HECHE: MSAJILI HANA MAMLAKA YA RUFAA
Akiwa amejaa hisia kali, Heche alimtuhumu Msajili kwa kutumia mamlaka yake kinyume cha sheria kwa kutaka kuingilia taratibu za ndani za Chadema, akisema:
“Msajili siyo mamlaka ya rufaa kwenye chama chetu. Chama chetu kina vyombo vyake vya kushughulikia malalamiko. Kama mtu ana malalamiko, arudi ndani ya chama, asikimbilie kwa Msajili.”
Heche alifichua kuwa kuna njama nyingi zimekuwa zikifanyika dhidi ya Chadema, ikiwemo matumizi ya wanachama wa zamani kuwasilisha barua kwa Msajili wakipinga uchaguzi uliofanyika hadharani na kurushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari.
“Wakaandika barua mwezi Machi, wakaipa Msajili. Halafu wakamtumia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar kufungua kesi eti kwamba chama kinadhulumiwa kutoka Bara,” alisema.
Aidha, Heche alieleza kuwa hatua ya Msajili kusitisha ruzuku na kutishia kukifuta chama hicho ni ukiukaji wa sheria:
“Msajili anasema anakifutia Chadema ruzuku, anatishia kukifuta chama hiki kinyume na utaratibu wa sheria. Hatuwezi kukubali,” alisema kwa msisitizo.
“SITAKIMBIA NCHI HII” – HECHE
Katika hotuba yake yenye kuchochea hamasa, Heche alisisitiza kuwa hataogopa vitisho:
“Nimeambiwa niangalie sana namba zangu zinahesabika... lakini nawaambia, sitakimbia nchi hii hata dakika moja. Kama damu yangu itamwagika katika kutetea haki, imwagike. Tusiwe waoga.”
MNYIKA: TUKO TAYARI UCHAGUZI UAHIRISHWE
Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema wao kama chama wako tayari kuona uchaguzi ukiahirishwa ili kutoa nafasi kwa kufanyika kwa mabadiliko ya msingi kwenye tume ya uchaguzi.
“Tunasema imetosha damu kumwagika kwenye chaguzi. Tuko tayari uchaguzi usogezwe mbele hadi mabadiliko ya sheria na katiba yafanyike kuliko kwenda kwenye uchaguzi kinyume na haki,” alisema Mnyika.
Akiwakumbusha wananchi historia ya Arusha, Mnyika alitaja matukio ya miaka 2010 na 2013 ambapo watu walifariki kutokana na vurugu wakati wa chaguzi.
LEMA: TUNAHAMASISHA UMOJA NA UJASIRI
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, Godbless Lema, alisema kuwa mfumo wa utawala uliopo unawapora wananchi haki yao ya kuungana na vyama vya upinzani:
“Kiongozi yeyote wa sasa — Mkuu wa Mkoa, Wilaya, Polisi — wote wanapigania maslahi ya chama tawala. Tunataka mabadiliko. Tumezuiwa kufanya mikutano kama vile ni kosa la jinai,” alisema Lema.
Aliwataka wananchi wa Arusha kuendelea kushiriki kikamilifu katika operesheni ya kudai mabadiliko:
“Tusiogope. Hakuna kurudi nyuma. Tuchangie chama chetu na tuunge mkono harakati hizi,” alisisitiza.
JACOB: TUKO PAMOJA SASA
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, alikanusha taarifa za mgawanyiko ndani ya chama:
“Nimekuja kusimama hapa kama ishara ya umoja. Propaganda kuwa hatuko pamoja si kweli. Baada ya uchaguzi, sisi sote tuko nyuma ya aliyeshinda.”
DKT SLAA: NYIE NI KIZAZI CHA UKOMBOZI MPYA
Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, aliwapongeza Heche na Lissu kwa kuongoza harakati za sasa:
“Heche na Lissu mmeanzisha historia mpya. Kama alivyoanza Mwalimu Nyerere na ukombozi wa kwanza, nyie mnaongoza ukombozi wa pili. Msiogope, huu ndio wakati wa kuiondoa CCM madarakani.”
MAHINYILA: HATUTEKELEZI AMRI ZA MSAJILI
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) Taifa, Deogratias Mahinyila, alisema:
“Hatufanyi kazi kwa maelekezo ya Msajili. Tutatekeleza mambo ya chama kwa ratiba yetu wenyewe.”
“No reforms, no election.”







0 Comments:
Post a Comment