“TUMEACHWA NJE KAMA WAKIMBIZI” — WAKAZI WA OLOSIVA WALIA NA BOMOA BOMOA ISIYOFUATA SHERIA


Wadai kutopata taarifa, Wabomolewa bila fidia, licha ya kumiliki maeneo kisheria



Wakazi wa Kitongoji cha Olosiva, kata ya Olorien Wilayani Arumeru, wamejikuta kwenye hali ya majonzi, sintofahamu na taharuki kubwa kufuatia zoezi la bomoa bomoa lililofanyika Aprili 12, 2025, ambapo uzio wa nyumba zaidi ya 20 ulivunjwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni upanuzi wa barabara.



Wakizungumza na vyombo vya habari, wakazi hao wamedai kuwa zoezi hilo limefanyika bila kuwahusisha, wala kuwapatia taarifa rasmi, licha ya wao kumiliki maeneo hayo kihalali kwa hati halali za umiliki. 



Wamesema kuwa walishangazwa na kuamshwa asubuhi kwa kelele za mashine na watu waliokuwa wakivunja kuta za uzio, bila kufahamu kinachoendelea.



“Nimepata taarifa kuwa nyumba yangu imebomolewa, uzio nikiwa kazini. Sikuwa nimepatiwa taarifa yoyote. Wamefanya bomoa bomoa isiyo na taarifa kama vile mtu hana uhalali. 



Nilikuwa nakaa ndani ya nyumba yenye fensi ya ukuta na umeme, halafu leo niko nje kama hivi, usalama uko wapi?” alisema Glory Costa Maule kwa huzuni.



Glory alieleza kuwa alijenga uzio wa nyumba yake miaka 20 iliyopita kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 15, akitumia matofali magumu, waya wa umeme na nguzo imara. Kwa sasa, alibaki hana pa kuishi huku mali zake zikiwa zimeachwa wazi nje.

“Nalalaje kwenye njia panda? Mahali palikuwa na ukuta wenye nguzo zaidi ya kumi, halafu leo pako wazi. Vitu vyangu vyote viko nje. Ninaishi kama mkimbizi. 


Hii ni bomoa bomoa gani isiyo na taarifa kama vile sisi ni wavamizi? Mimi ni Mtanzania, na kila kitu ninachomiliki kiko kisheria. 


Hati ninazo, lakini hakuna aliyezingatia hilo,” aliongeza kwa uchungu.

Akiendelea kueleza, Glory alisema alipowauliza viongozi waliokuwa wakisimamia zoezi hilo kuhusu taarifa, alielezwa kuwa ni maamuzi ya mkutano wa wananchi, jambo ambalo linamshangaza kwani hakuwa amepewa taarifa wala kualikwa.

“Niliwauliza, kama kuna bomoa bomoa, mbona hakuna taarifa niliyopewa?


 Wakasema wananchi wameamua na wao ni viongozi wa wananchi. Nikauliza, hao wananchi wanaoamua ni kina nani wakati sisi tunamiliki maeneo kihalali na hatujapewa taarifa yoyote?”

Aliongeza kuwa taarifa ya bomoa bomoa hiyo ilisambazwa kupitia kundi la WhatsApp la kijiji, ambalo yeye si mwanachama wake.


“Hata jirani zangu hawakupata taarifa rasmi. Mmoja tu alisema aliona kwenye grupu la WhatsApp la kijiji. Sasa taarifa rasmi ni lazima iwe ya maandishi, si ya mitandaoni,” alisema Glory.


Rose Swai, mkazi mwingine wa Olosiva, alisimulia tukio hilo kwa uchungu na kusema kuwa aliamshwa alfajiri kwa kelele za watu waliokuwa wakivunja kuta za uzio wa nyumba yake.


“Nilikuwa nimelala alfajiri, nimeshtushwa na kelele nje. Nilipotoka, nikakuta watu wanavunja uzio wa nyumba. Tulipowauliza mnavunja nini?. Diwani na mwenyekiti wakasema watu wanaoishi kwenye nyumba iliyo kwenye mstari wa uzio watoe vitu vyao ili pavunjwe,” alisema Rose.

Rose alisema kuwa licha ya kuwa mpangaji halali aliyelipa kodi ya miezi minne, hakupewa taarifa ya zoezi hilo mapema.


“Nimelipa kodi ya miezi minne. Kama ni kuondoka, nilipaswa kupewa taarifa mapema. Siwezi kuondoka ghafla niseme naenda kutafuta nyumba nyingine. Sina hela ya kuhama ndani ya siku saba,” alilalamika.


Kwa upande wa viongozi, Diwani wa Kata ya Olorien, Erick Semboja, alithibitisha kuwa zoezi hilo lilitekelezwa kwa mujibu wa maamuzi ya mkutano wa wananchi na kwamba lengo ni kupanua barabara zilizojengwa kiholela.



“Jumla ya nyumba 20 tumevunja kuta zake za uzio ambazo ziliingia ndani ya barabara. Wapo wengine tuliowapa muda zaidi wa kuondoka baada ya kuelewa umuhimu wa zoezi hili. Hatutaki kutumia nguvu kwa mtu yeyote aliye tayari kushirikiana,” alisema Diwani Semboja.

Aliongeza kuwa:
“Olosiva kuna barabara kuu tatu. Tumeshafanya kazi kwenye barabara ya KKKT. Tutafuata barabara ya Katoliki, kisha Njia Ng’ombe. Tutachimba mitaro, tupanue barabara. Haiwezekani kila siku kero iwe barabara.”


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olosiva, Naishiye Kimani, naye alieleza kuwa wakazi walipatiwa barua kuhusu mpango huo mara tu baada ya yeye kuingia madarakani.

“Nilipoingia madarakani, (2024) kila mmoja tulimpa barua kuhusu mipango ya barabara. Hili si jambo la ghafla,” alisema Kimani.

Kuhusu fidia kwa walioathirika, Kimani alisema:
“Hakuna fidia kwa sababu maeneo haya yaliuzwa na wananchi wenyewe. Wananchi sasa wameamua warudishe barabara zao walizokuwa nazo awali.”

Hata hivyo, kauli hizo zimepingwa vikali na wakazi waliobomolewa ambao wameeleza kuwa hawakuwahi kupokea barua wala kushiriki katika uamuzi wa aina hiyo. Wameiomba serikali kuu kuingilia kati, wakisisitiza kuwa haki na sheria havikuzingatiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo.


“Tunaomba serikali kuu iingilie kati. Hatuwezi kuachwa hivi tu kana kwamba hatuna haki. Tumenyimwa taarifa, tumebomolewa nyumba, na sasa tunaishi nje bila msaada wowote,” alisema Glory kwa uchungu.

0 Comments:

Post a Comment