CHADEMA Yapinga Marufuku ya INEC, Yasema Uamuzi Unakiuka Katiba

 

Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, kimepinga vikali uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wa kukipiga marufuku kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na chaguzi nyingine zote ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

INEC ilitoa tamko hilo Jumapili iliyopita, ikieleza kuwa CHADEMA imeshindwa kutia saini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, jambo ambalo limeelezwa kuwa kigezo cha kukiondoa chama hicho kwenye orodha ya vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo. 


Hata hivyo, CHADEMA kinasema kuwa hatua hiyo haina msingi wa kikatiba na ni kinyume cha sheria.





Akizungumza leo Aprili 15, 2025 jijini Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Rugemeleza Nshala, alisema:

“Haki ya kuchaguliwa kuwa mgombea inatolewa na Katiba. Alichokisema Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ni kosa kubwa – limekiuka sheria ya nchi, limekiuka Katiba, na limekiuka hata kanuni ambazo hazijaanza kufanya kazi. Mtu anabanwaje na kanuni ambazo hazijaanza kufanya kazi?”

Akiendelea, Dkt. Nshala alimkosoa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, kwa kile alichokiita propaganda zisizo na msingi:

“Ndugu Kailima, tafadhali naomba ujitazame mara mbili, kasome kanuni vizuri uone usahihi wa maneno yako. Kilichofanywa ni propaganda chafu. Tunataka kama dhamira zao ni safi na akili zao zinafanya kazi, wafute hilo tamko. Kailima amekosea na anatakiwa kutoka hadharani na kufuta kauli yake.”

“CHADEMA haijabadilisha msimamo wake – bado tunasisitiza mageuzi ya uchaguzi. Sisi msimamo wetu uko palepale: No reforms, no election.

Kwa upande wake, Kiongozi wa chama hicho, Tundu Lissu, ambaye alikamatwa wiki iliyopita na kufunguliwa mashtaka ya uhaini, aliwahi kueleza kuwa CHADEMA haiwezi kushiriki katika uchaguzi wowote bila kufanyika kwa mageuzi ya msingi kwenye mfumo wa uchaguzi.

“Huu uchaguzi ulivyo bila reforms, tukiingia tumepigwa. CCM ni kama wamechukua madume na majike yote, kwa hiyo wewe ukienda, umepigwa. Ni set up game. Hatuwezi kuwa na viongozi wanaotokana na uhuni na wizi wa kura. Hatuwezi kuwa na uchaguzi wa ujanja ujanja – haikubaliki,” alisema Lissu.

CHADEMA inasisitiza kuwa haki ya kushiriki uchaguzi ni ya kikatiba na haiwezi kuzuiwa kwa kigezo cha kutosaini kanuni ambazo bado hazijaanza kutumika. Chama hicho kimeitaka INEC kufuta mara moja tamko lake na kuheshimu misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

0 Comments:

Post a Comment