Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki na kutimiza matakwa ya kimataifa katika kupambana na kudhibiti uhalifu wa kifedha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani kwa viwango vinavyotambulika kimataifa.
Akizungumza leo Jumatatu, Aprili 14, 2025, wakati wa ufunguzi wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu (FATF), uliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema:
“Tanzania inatambua changamoto za uhalifu wa kifedha na imejidhatiti katika kudhibiti hali hiyo kwa viwango vya kimataifa vilivyopo.”
Ameongeza kuwa tathmini zilizofanywa na taasisi za Kuthibiti Uhalifu wa Kifedha Kusini Mashariki mwa Afrika mwaka 2021, pamoja na ile ya Kikosi cha Kimataifa cha Ushirikiano na Tathmini ya mwaka 2022, zimeiwezesha Tanzania kuimarisha uwezo wa mapambano dhidi ya fedha haramu.
“Tumeimarisha mifumo ya kupambana na fedha haramu kwa kujengea uwezo rasilimali watu na vifaa taasisi zinazohusika. Pia tumeweka mkazo katika mabadiliko ya sheria na sera, matumizi ya takwimu na teknolojia, pamoja na kuimarisha sekta ya nyumba na ardhi,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa hatua zilizochukuliwa na Tanzania zimekuwa na matokeo chanya katika kudhibiti uhalifu wa kifedha.
“Baada ya kupokea mpango kazi kutoka Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kupambana na Fedha Haramu, Tanzania ilifanya maamuzi ya ngazi ya juu ya kuimarisha usimamizi wa uhalifu wa kifedha nchini, hali ambayo imeonesha mafanikio makubwa,” amesema Dkt. Nchemba.
Mkutano huo unalenga kufanya tathmini ya hatua zilizopigwa na Tanzania katika utekelezaji wa mapendekezo ya kimataifa ya kudhibiti fedha haramu na kufungua fursa zaidi za ushirikiano wa kimataifa katika mapambano hayo.





0 Comments:
Post a Comment