Menejimenti ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imeweka vipaumbele muhimu katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii nchini.
Pamoja na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya utalii na utawala ikiwemo matengenezo ya barabara zilizopo hifadhini, ujenzi wa malango ya utalii na ujenzi wa hosteli zinazotumiwa na wanafunzi wanapotembelea Hifadhi za Taifa, Shirika limejizatiti kuongeza nguvu katika masuala ya ulinzi na usalama wa hifadhi.
Aidha, lengo ni kuboresha upatikanaji wa vitendea kazi, pamoja na kununua magari ya doria na kukarabati magari mengine yaliyoharibika.
Kamishna wa Uhifadhi, Juma Nassoro Kuji, ambaye aniongoza Menejimenti hiyo, alisema kuwa bajeti hiyo itahusisha kuanzishwa kwa mazao mapya ya utalii, lengo likiwa ni kuongeza mapato kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.
Alizungumzia pia umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika shughuli za uhifadhi, matumizi ya teknolojia za kisasa, pamoja na utatuzi wa migogoro inayojitokeza kati ya wanyamapori na binadamu.
"Vipaumbele vya bajeti hii vimejikita katika kuboresha usalama wa maeneo yetu ya hifadhi, kujenga miundombinu bora, na kuhakikisha kuwa tunapata vifaa vya kisasa vinavyohitajika kwa ajili ya shughuli za uhifadhi," alisisitiza Kamishna Kuji.
Pia, Kamishna Kuji alieleza kuwa wataendelea kudhibiti mimea vamizi, wanyamapori wakali na waharibifu, na kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii. Aliongeza kuwa bajeti hiyo pia inakusudia kutatua changamoto zinazohusiana na wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na kuboresha maslahi ya watumishi wa Shirika.
Vipaumbele hivi vilijadiliwa katika kikao kazi cha Menejimenti ya Shirika kilichofanyika Aprili 4, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Hifadhi ya Taifa ya Manyara.
Kikao hicho kilijikita katika maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo Kamishna Kuji alieleza dhima ya Shirika katika kutengeneza bajeti inayoangazia masuala muhimu ambayo yatachangia kufikiwa kwa malengo ya uhifadhi na utalii.
"Wajumbe wa kamati ya bajeti ya Shirika walipata fursa ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025. Katika ripoti hiyo, walibainisha maeneo muhimu ambayo yametekelezwa kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha Watanzania kuchangamkia fursa ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea Hifadhi za Taifa na Vituo vya Malikale vilivyokasimishwa kwa TANAPA," alifafanua Kamishna Kuji.
Aidha, Kamati hiyo ilieleza kuwa maeneo mengine muhimu ya kuwekeza ni pamoja na maboresho ya miundombinu ya utalii, ujenzi wa malango ya utalii, na ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotembelea hifadhi za taifa.
Alisisitiza pia kuwa wataendelea kudhibiti mimea vamizi, wanyamapori wakali na waharibifu, na kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii.
Mapendekezo ya Bajeti ya Shirika kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yatawasilishwa kwa ngazi mbalimbali za maamuzi kwa ajili ya uchambuzi na idhini kabla ya kuanza kutumika rasmi mnamo tarehe 1 Julai 2025.
Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kuhakikisha uhifadhi endelevu wa maeneo yote yaliyotengwa kuwa hifadhi za Taifa nchini, ili kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
0 Comments:
Post a Comment