Waziri Gwajima Alaani Vikali Mabinti Kumdhalilisha Mwanafunzi Mwenza Kisa Mwijaku, Aagiza Hatua za Kisheria

 



Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amelaani vikali tukio la udhalilishaji lililofanywa na wasichana kadhaa dhidi ya msichana mwenzao, huku wakiandaa na kusambaza video ya tukio hilo katika mitandao ya kijamii. Wasichana hao, ambao ni wanafunzi kutoka vyuo viwili tofauti vya elimu ya juu nchini, wanadaiwa kumshambulia kwa maneno na vipigo msichana huyo kwa sababu ya ugomvi wa mapenzi.



Katika taarifa yake aliyoitoa leo Aprili 20, 2025, Dkt. Gwajima alisema, “Usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka tarehe 20 Aprili, 2024 nilipokea tags nyingi kupitia mtandao wa Instagram wakinitumia video kadhaa zinazoonesha Mabinti kadhaa wakishirikiana kumdhalilisha Binti mwingine kwa maneno na vipigo na mambo mengine mabaya, kwenye mazungumzo yao kama yanavyosikika, inaonekana ni ugomvi wa kumgombania Mwanaume anayetajwa kwa jina moja la Mwijaku.”





Dkt. Gwajima alieleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo na kusema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wasichana walio katika mazingira ya kujifunza na kujenga maisha yao wakijihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya wenzao.

“Binafsi, nimesikitishwa sana kusikia Mabinti wasomi ambao, wangetakiwa kujikita kwenye elimu na kuunganisha nguvu kupambana kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto badala yake wanatumia nguvu zao na elimu zao kukatiliana, kudhalilishana na kujidhalilisha wao kwa wao,” alisema.

Ameeleza kuwa tayari ameweza kuwasiliana na manusura wa tukio hilo na kuhakikisha anapatiwa huduma muhimu ikiwemo msaada wa kisaikolojia, huduma za ustawi wa jamii pamoja na msaada wa kisheria kupitia Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi.

“Nimewasiliana na manusura na kumuunganisha na huduma za ustawi wa jamii, msaada wa kisaikolojia na huduma za Dawati la Jinsia Polisi ambapo, pia atapata msaada wa kisheria ili haki itendeke, nawasiliana na Wakuu wa Vyuo husika kupitia Madawati ya Jinsia kwenye Vyuo husika ili hatua za nidhamu zichukuliwe kupitia Sheria na Miongozo ya Vyuo husika dhidi ya waliofanya udhalilishaji huu,” aliongeza.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema anaendelea kuwasiliana na viongozi wa sekta nyingine husika kwa hatua zaidi.

“Nawasiliana na Waziri mwenye Dhamana na Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi, wito kwa Wananchi kwa ujumla ikiwemo Wanafunzi wa ngazi mbalimbali, tuache kumaliza migogoro kupitia utaratibu wa kudhalilisha wengine,” alisema.

Katika hitimisho la taarifa yake, ametoa wito kwa wanawake wote nchini kushikamana katika kulinda heshima yao na kupinga ukatili wa kijinsia.

“Aidha Wanawake wenzangu wote, hima tulinde heshima na haiba yetu kwa kuungana kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa Watoto huku sisi wenyewe tukijitenga na hatua za kukatili na kudhalilisha wengine.”

0 Comments:

Post a Comment