MAJALIWA AIPONGEZA TANAPA KWA MCHANGO MKUBWA KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA UTALII NCHINI





Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa, amelitaja Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kama moja ya taasisi muhimu katika maendeleo ya sekta ya utalii nchini kutokana na mchango wake mkubwa katika uhifadhi na kukuza utalii.


Hii ni baada ya kuzindua lango jipya la utalii la Ndea, lililopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi katika Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro, Machi 25, 2025. 



Lango hilo limejengwa kimkakati kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha miundombinu ya utalii.


"Leo tunazindua lango la Ndea kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Lango hili limejengwa kimkakati kwani lipo karibu na majirani zetu wa Hifadhi ya Tsavo iliyopo nchini Kenya ambapo ni karibu na Hifadhi ya Taifa Mkomazi. 


Hivyo, uimarishaji wa miundombinu hii ya utalii utasaidia kupokea watalii watakaotokea nchini Kenya na kuingia Hifadhi ya Taifa Mkomazi kujionea vivutio mbalimbali ikiwemo faru weusi," alisema Majaliwa.



Waziri Mkuu aliendelea kwa kumpongeza TANAPA kwa juhudi zake kubwa za kuboresha sekta ya utalii na uhifadhi nchini. Alisema kuwa maboresho hayo yanaonekana kwa namna ambavyo wananchi hasa wa maeneo jirani na hifadhi wanavyoanza kunufaika.


"Niwapongeze TANAPA kwani ninyi ni taasisi kubwa nchini katika masuala ya uhifadhi na utalii, na mmekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya utalii hapa nchini. Tumeshuhudia TANAPA ikifanya maboresho makubwa kwenye sekta ya uhifadhi na utalii na matokeo yake tumeanza kuyaona yanavyonufaisha wananchi hasa waliopo karibu na maeneo ya hifadhi zetu," alisisitiza Waziri Mkuu.



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliainisha faida zitakazopatikana kutokana na uzinduzi wa lango hilo. 


Alisema kuwa lango hilo litasaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Mwanga, hasa kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazozalika kutokana na biashara ya utalii.


"Kwa kweli, lango hili litakuwa na manufaa makubwa. Litaongeza uchumi wa wananchi wetu hasa wale wa Wilaya ya Mwanga kupitia mnyororo wa thamani wa biashara ya utalii. Watalii wengi kutoka Kenya watakuwa na urahisi wa kufika hapa na kujiunga na utalii wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi," alifafanua Mkuu wa Mkoa.



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Juma Kuji, alizungumzia umuhimu wa mradi huo na kumshukuru Waziri Mkuu kwa kushiriki katika uzinduzi huo. Alisema kuwa lango hilo ni sehemu muhimu ya kuboresha miundombinu ya utalii na kwamba utakuwa na manufaa kwa wananchi wa Wilaya ya Mwanga, hasa wale wa Tarafa ya Jipe Ndea.


"TANAPA tunatoa pongezi kwako, Kasim Majaliwa, kwa kuja katika eneo la mradi na kuzindua rasmi geti hili ambalo litakuwa na faida nyingi. Litaimarisha uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Mwanga, hususani wale wa Tarafa ya Jipe Ndea, na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hii. 


Pia, lango hili litakuwa na miundombinu ya ulinzi wakiwemo askari na vitendea kazi vyao watasaidia kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo, pamoja na kuboresha mahusiano kati ya hifadhi na jamii," alisema Kamishna Kuji.





Kwa upande mwingine, Kamishna Kuji aliongeza kuwa Serikali kupitia Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetekeleza jumla ya miradi kumi na moja (11) ndani ya hifadhi hiyo na maeneo jirani.


 Alibainisha kuwa mradi wa ujenzi wa lango la Ndea umegharimu jumla ya shilingi milioni 350 na umehusisha ujenzi wa lango dogo, ofisi, choo cha wageni chenye matundu matano, ujenzi wa barabara ya kilometa 4.5, pamoja na uwekaji wa mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki.


Lango la Ndea lipo ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi, jirani na Kijiji cha Karambandea, katika Kata ya Toloha, Tarafa ya Jipe Ndea, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro. Lango hili linatarajiwa kutoa fursa za kiuchumi na kuimarisha sekta ya utalii katika eneo hilo.


0 Comments:

Post a Comment