Vatican, Aprili 21, 2025 — Dunia imeguswa na msiba mkubwa kufuatia tangazo rasmi kutoka Vatican kuhusu kifo cha Baba Mtakatifu Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani. Tangazo hilo lilitolewa leo saa 3:45 asubuhi (saa za Rome) na Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Chumba cha Kitume, akiwa katika makaazi ya Papa, Casa Santa Marta.
Kwa sauti ya huzuni, Kardinali Farrell alisema:
“Ndugu wapendwa, kwa huzuni kubwa natangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francis. Saa 1:35 asubuhi hii, Askofu wa Roma, Francis, amerudi nyumbani kwa Baba. Maisha yake yote yalikuwa ya kumtumikia Bwana na Kanisa Lake. Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu mzima, hasa kwa ajili ya maskini na waliotengwa. Kwa shukrani kuu kwa mfano wake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunakabidhi roho ya Papa Francis kwa upendo wa huruma usio na mipaka wa Mungu mmoja wa Utatu Mtakatifu.”
Historia ya Ugonjwa Wake
Papa Francis alilazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli mnamo Ijumaa, Februari 14, 2025, baada ya kuugua kwa siku kadhaa kutokana na maambukizi ya mfumo wa upumuaji (bronchitis). Mnamo Februari 18, madaktari waligundua kuwa alikuwa anaugua pneumonia ya mapafu yote mawili (bilateral pneumonia), hali iliyopelekea afya yake kuzorota zaidi.
Baada ya siku 38 hospitalini, aliruhusiwa kurejea Vatican na kuendelea kupata matibabu na mapumziko nyumbani katika makaazi ya Casa Santa Marta. Hata hivyo, afya yake iliendelea kudhoofika hadi kufikia kifo chake leo.
Papa Francis alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kupumua kwa miaka mingi. Mnamo mwaka 1957, akiwa kijana nchini Argentina, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa sehemu ya mapafu kutokana na maambukizi makali. Katika miaka ya hivi karibuni, mara kadhaa alifuta shughuli za kimataifa kwa sababu ya matatizo ya afya, ikiwemo ziara aliyopaswa kufanya katika Umoja wa Falme za Kiarabu mnamo Novemba 2023.
Mazishi Yake na Toleo Jipya la Ibada
Mnamo Aprili 2024, Baba Mtakatifu Francis aliridhia toleo jipya la kitabu cha liturujia kwa ajili ya mazishi ya Kipapa lijulikanalo kama Ordo Exsequiarum Romani Pontificis. Toleo hili linaelekeza kuwa uthibitisho wa kifo hufanyika katika kapela, na mwili wa Papa huwekwa moja kwa moja kwenye jeneza, badala ya taratibu zilizotumika awali.
Askofu Mkuu Diego Ravelli, Mwalimu wa Sherehe za Kipapa, alisema:
“Ibada mpya iliyosasishwa inalenga kuonyesha kwa nguvu zaidi kwamba mazishi ya Papa wa Roma ni ya mchungaji na mfuasi wa Kristo, na si ya mtu mwenye nguvu za dunia hii.”
“Papa Francis aliomba mazishi yake yafanyike kwa unyenyekevu na yalenge zaidi imani ya Kanisa katika mwili wa Kristo aliyefufuka.”
Mpaka sasa, tarehe rasmi ya ibada ya mazishi bado haijatangazwa, lakini inatarajiwa kufanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa mujibu wa mila na desturi za Kanisa Katoliki.
Baba Mtakatifu Francis atakumbukwa kama kiongozi wa kiroho aliyejitoa kwa dhati kwa maskini, amani, na mshikamano wa binadamu kote duniani.

0 Comments:
Post a Comment