Majaliwa Aagiza Ukaguzi wa Mara kwa Mara Madaraja na Makalavati Nchini



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametoa agizo kwa Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye madaraja na makalavati ya barabara kuu nchini ili kuzuia athari zitokanazo na mvua zinazoendelea kunyesha.



Agizo hilo limetolewa leo, Jumatano Aprili 16, 2025, wakati Waziri Mkuu alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati wa madaraja yaliyokatika kutokana na mvua katika maeneo ya Matandu na Somanga Mtama, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi.



“Fedha ambayo tunatenga kwa ajili ya ukarabati itumike ipasavyo. Kila baada ya mvua kubwa kunyesha, wakajiridhishe na kama kipenyo cha daraja na makalavati yapo vilevile,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi kuhakikisha kazi za ukarabati zinafanyika usiku na mchana ili kurejesha maeneo yote yaliyoathirika na mvua katika hali yake ya kawaida.



Amebainisha kuwa Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kujenga upya barabara ya Dar es Salaam – Lindi – Mtwara kwa kiwango cha juu. “Tumetenga fedha ya ujenzi wa kilomita 100. Tumefanya hivi ili kuepuka kuweka viraka viraka, badala yake tujenge upya eneo lote korofi.”

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewahakikishia watumiaji wa barabara hiyo kuwa shughuli zote muhimu zitaendelea kama kawaida huku Serikali ikiendelea kufuatilia kwa karibu uimarishaji wa miundombinu hiyo. “Lengo ni kuhakikisha Serikali ipo kazini, na imeshaleta wakandarasi. Hii ni kutokana na maelekezo ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.”

Amesema kuwa Rais Dkt. Samia tayari ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vipande vya barabara vilivyoharibiwa na mvua katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema: “Mpaka sasa mkandarasi ameshaweka nguzo 23 kati ya 43 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu kwenye eneo la Somanga.”

0 Comments:

Post a Comment