Ujenzi wa Barabara za Lami Waongezeka kwa Asilimia 71 katika Bajeti ya 2024/25


Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya barabara nchini kwa kasi kubwa, ambapo ujenzi wa barabara za lami na changarawe umeongezeka kwa kiwango kikubwa kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25.



Akizungumza leo Aprili 16, 2025 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema kuwa urefu wa barabara za vijijini na mijini zilizojengwa kwa kiwango cha lami umeongezeka kutoka kilomita 2,025 hadi kilomita 3,467.30, sawa na asilimia 71.22.



Tulipotoka kulikuwa na vumbi, lakini leo tunatembea kwenye lami. Tulipotoka kulikuwa na miteremko isiyopitika, leo tuna barabara zinazounganisha ndoto na fursa,” amesema Mchengerwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2025/26.



Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara za changarawe umeongezeka kutoka kilomita 24,493 hadi kilomita 44,372.21, sawa na ongezeko la asilimia 81.16, huku mtandao wa barabara nchini ukiongezeka kutoka kilomita 108,946.19 hadi 144,429.77, sawa na asilimia 32.57.

Kuongezeka kwa barabara za changarawe kwa asilimia 81.16 na lami kwa asilimia 71.22 ni ushahidi wa nchi inayojenga msingi wa maendeleo kwa kila Mtanzania, kuanzia kijijini hadi mjini. Huu sio mradi wa barabara tu, huu ni mradi wa matumaini,” amesema.

Kuhusu matumizi ya teknolojia mbadala, amesema kuwa barabara zenye urefu wa kilomita 61.7 zinaendelea kufanyiwa tafiti ili kupunguza gharama za ujenzi, matengenezo na ukarabati.



Amefafanua kuwa barabara siyo tu njia ya usafiri bali ni kiunganishi muhimu katika maisha ya kila Mtanzania.

Kila kilomita moja ya barabara ni daraja kati ya umasikini na maendeleo. Ni njia ya mtoto kufika shuleni, mama kufika hospitali, mkulima kupeleka mazao sokoni na taifa kusonga mbele,” amesema Mchengerwa.

Amesisitiza kuwa ongezeko la mtandao wa barabara kutoka kilomita 108,946 hadi zaidi ya kilomita 144,000 ni mabadiliko halisi na si takwimu tu.

Barabara hizi ni sauti ya Serikali inayosema: ‘Hatukuwaacha nyuma.’ Hizi ni njia zinazotufikisha kwenye Tanzania ya viwanda, fursa na mshikamano,” amesema.



Katika bajeti ya mwaka 2024/25, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) iliidhinishiwa shilingi bilioni 908.16 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara. Hadi kufikia Machi 2025, shilingi bilioni 468.40 zilikuwa zimetolewa, sawa na asilimia 55.68 ya fedha zilizoidhinishwa.

0 Comments:

Post a Comment