Biden Akosoa Mwelekeo wa Serikali Mpya katika Sera za Ustawi wa Jamii

 


Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden, ameikosoa vikali serikali ya sasa kwa kile alichokiita "mwelekeo wa kikatili" katika Idara ya Ustawi wa Jamii. 


Akizungumza katika mkutano uliofanyika mjini Chicago, Biden alisema kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali hiyo mpya zimeleta madhara makubwa kwa wananchi wanaotegemea huduma hizo.

"Katika muda usiozidi siku 100, utawala huu mpya umefanya uharibifu mkubwa na mabaya mengi. Ni jambo la kusikitisha," alisema Biden bila kumtaja Donald Trump kwa jina.

Katika hotuba hiyo, ambayo ilikuwa ya kwanza tangu kuondoka kwake madarakani, Biden alisisitiza kuwa mfumo wa ustawi wa jamii unahitaji kulindwa na kuboreshwa badala ya kupunguzwa. Alitoa kauli hizo wakati wa hafla maalum ya haki za walemavu.

Serikali mpya, ikiwemo Donald Trump na mfanyabiashara Elon Musk, imedai kuwa mfumo huo wa ustawi wa jamii unakumbwa na udanganyifu, na wameonyesha nia ya kuupunguza ili kupunguza gharama za serikali.

Hata hivyo, Biden hakugusia suala la kuondoka kwake Ikulu ya White House wala kutoa maoni kuhusu uchaguzi wa rais wa 2024.

Wanasiasa wa chama cha Democratic wameendelea kuushutumu utawala wa sasa kwa mipango yake ya kupunguza ufadhili kwa huduma za kijamii, wakisema hatua hiyo inawaathiri moja kwa moja watu wenye uhitaji mkubwa.

0 Comments:

Post a Comment