CAG Abaini Malipo ya Ziada ya Sh. Milioni 586.43 kwa Wakandarasi TANROADS

 


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kuwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ulilipa malipo ya ziada kwa wakandarasi yenye thamani ya Shilingi milioni 586.43 kinyume na masharti ya mikataba ya miradi husika.

Katika ripoti yake ya ukaguzi, CAG amesema mnamo Agosti 1, 2023, TANROADS ililipa kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Company (CCECC) jumla ya Shilingi 3,894,793,405.21 kwa ajili ya malipo ya awali ya Mkandarasi namba 1 (IPC Na. 1) chini ya Mradi wa Ushirikiano wa Usafiri Tanzania (TanTIP).

“Hata hivyo, katika malipo haya, nilibaini malipo ya ziada ya jumla ya Shilingi 540,792,094 yaliyotokana na matumizi yasiyo sahihi ya fomula ya marekebisho ya bei,” amesema CAG.

Aidha, katika ukaguzi wa Mradi wa Barabara ya Mkoa wa Iringa (Ipogolo - Kilolo), CAG aligundua malipo ya ziada ya Shilingi 45,640,034 yaliyotokana na madai ya malipo ya wakandarasi namba 2 na 3.

Katika kiasi hicho, Shilingi 9,462,996 zilihusiana na uchimbaji wa miamba ambayo tayari ilikuwa imelipwa kwenye ankara za nyuma, Shilingi 18,743,120 zilikuwa ni gharama za vipimo vya maabara ambazo zilipaswa kulipwa na mkandarasi, na Shilingi 17,433,918 zilithibitishwa kimakosa kama ada ya Bodi ya Kuepusha/Kusimamia Migogoro (DAAB).

“Ninapendekeza menejimenti ya TANROADS ipitie upya mchakato wa malipo na kuhakikisha kuwa hesabu za marekebisho ya bei zinazingatia kwa makini masharti ya mkataba, hususani matumizi sahihi ya fomula kama ilivyoainishwa katika kifungu kidogo cha 3.7.2 cha masharti ya jumla ya mkataba,” amesema CAG.

Aidha, CAG ametoa wito kwa TANROADS kuwawajibisha wakandarasi waliolipwa fedha zaidi na kuhakikisha wanarejesha kiasi hicho, sambamba na kutekeleza mfumo madhubuti wa uthibitishaji wa hesabu kabla ya kuidhinisha malipo katika miradi inayofuata.

0 Comments:

Post a Comment