Kama umekuwa ukisumbuliwa na tatizo la kipara au changamoto ya nywele kung’oka, basi kuna habari njema kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) baada ya kugundua dawa ya asili ya kuotesha nywele au kuzuia nywele kutoka, dawa inayotokana na mmea uitwao Mporojo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi wa Utafiti wa TAWIRI, Dk. Julius Keyyu, amesema taasisi hiyo imefanya utafiti kwa kipindi cha miaka 12 na kufanikisha ugunduzi huo muhimu.
“Utafiti huu ulianza mwaka 2013 na umekamilika mwaka huu 2025, ambapo tulichunguza mimea ya tiba asili inayotumika na jamii mbalimbali katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania, hasa Wilaya za Ngorongoro, Mbulu na Hanang,” amesema Dk. Keyyu.
Ameeleza kuwa utafiti huo ulihusisha jamii za Kimasai, Hadzabe, Datoga na Iraqw ambao hutumia mmea wa Mporojo katika tiba zao za asili.
“Tuligundua kuwa mmea huu hausaidii tu kwenye tiba ya magonjwa mbalimbali, bali una uwezo mkubwa wa kuotesha nywele au kuzuia nywele zisikatike au kung’oka,” amesema Dk. Keyyu.
Amesisitiza kuwa dawa hiyo tayari imepata hati miliki na hatua zinazofuata ni kuhakikisha inaingia sokoni kwa matumizi ya Watanzania na dunia kwa ujumla.
“Tunachukua hatua kuhakikisha bidhaa hii salama na ya asili inasambazwa kwa njia rasmi baada ya taratibu zote kukamilika,” amesema.
Ugunduzi huu ni hatua muhimu katika kuimarisha tiba asili na kuonyesha mchango mkubwa wa utafiti wa kisayansi unaofanyika hapa nchini.

0 Comments:
Post a Comment