Katika kile kinachoonekana kuwa ni mgawanyiko wa wazi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kundi la wanachama wanaojiita G55 limetangaza msimamo wake hadharani kuhusu hatua ya chama hicho kutoshiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, likieleza kuwa hatua hiyo ni ya kujimaliza kisiasa na kuiua kabisa ndoto ya mabadiliko waliyoijenga kwa miaka mingi.
Akizungumza kwa niaba ya kundi hilo, John Mrema ambaye ni mmoja wa wanasiasa wa muda mrefu ndani ya chama, amesema kuwa:
“Pasaka yote hii, viongozi wa dini wote wanaunga mkono mabadiliko (reforms), lakini hakuna hata mmoja aliyesema tukazuie uchaguzi, wote wanatuhimiza waumini wakashiriki uchaguzi lakini wanaitaka serikali kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki, ndicho walichosema.
Sasa sisi kiburi chetu kinatuambia tukazuie uchaguzi, tukiulizwa tutazuiaje tunasema tunaingia barabarani… unakwenda kumzuia nani?” alihoji Mrema.
Akiendelea kueleza hali ya sintofahamu inayozidi kujitokeza miongoni mwa wanachama wa CHADEMA, Mrema alisema:
“Wako watu kwa maelfu na wengine wameshaanza kuondoka kwenye chama ndugu zangu… wako madiwani 85 wa kata wanauliza wafanye nini? Wanachama wenzetu tunawasihi mtulie kwa muda, wasifanye maamuzi, tuendelee kushauriana.”
Mrema alielezea pia msimamo wa G55 kuhusu hatua ya chama kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi, akisema:
“Jambo la pili ni chama chetu kutosaini kanuni za maadili ya uchaguzi na kukifanya sasa chama chetu kujiondoa rasmi kwenye uchaguzi. Jambo hili limeua ndoto za wanachama wa CHADEMA... ndoto zao zimekufa.”
Aidha, aliongeza kuwa hatua hiyo si tu imewakatisha tamaa wana-CHADEMA bali imewafanya wapoteze imani na mwelekeo wa chama hicho:
“Kanuni zimeshachapishwa kwenye gazeti la serikali, sasa ni rasmi kwamba CHADEMA haitashiriki uchaguzi mkuu wa 2025… watu hawa waliokuwa na ndoto za muda mrefu, ndoto zao zimeuawa kwa sababu tu ya kiburi cha viongozi wetu.”
Katika hatua nyingine, Mrema alilaani kile alichokiita tabia ya viongozi wa CHADEMA kutovumilia maoni mbadala:
“Tunakishauri tena chama (CHADEMA), utamaduni na njia hiyo wanayotaka kuchukua sasa (ya kufukuza wanachama) haitakiacha chama chetu salama… hivi ukipewa dola utasikiliza sauti za wapinzani wako kweli?”
Alikumbusha pia historia ya viongozi waliowahi kupinga maamuzi ya chama lakini hawakufukuzwa:
“Tundu Lissu, John Heche, Godbless Lema na Peter Msigwa waliendesha harakati kwamba chama kijitoe kwenye maridhiano… lakini hakuna aliyesema hawa watu tuwafukuze uanachama kwa sababu wanapinga maamuzi ya Baraza Kuu. Ni kwa sababu chama chetu kimejengwa kwenye misingi ya kusikiliza.”
Kwa mujibu wa Mrema, G55 itaendelea kushauriana na makundi mbalimbali ya wadau wa demokrasia ili kupata suluhisho la ndani na njia ya kurudisha matumaini kwa watanzania:
“G55 inaamini kwamba bado WanaCHADEMA wenyewe tunao uwezo na uhakika wa kupata ufumbuzi wa ndani wa changamoto zote za kidemokrasia zinazotukabili.”
Kauli hizi za Mrema na kundi la G55 zinakuja wakati CHADEMA ikiwa kwenye mchakato mgumu wa kujielekeza kisiasa baada ya kutangaza kutoshiriki uchaguzi, hali inayochochea hofu ya mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

0 Comments:
Post a Comment