Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa watumishi wa mizani ya barabara kutoka Tunduma (Songwe) hadi Vigwaza (Pwani) waliokuwa zamu Machi 13 mwaka huu, wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufuatia kuibuka kwa mvutano kati ya watumishi wa mzani wa Vigwaza na dereva wa magari makubwa ya mizigo aliyefahamika kwa jina la Pamela.
Katika picha mjongeo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ilionesha dereva huyo akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari ambapo alisimulia tukio hilo. Pamela, ambaye anafanya kazi kwenye kampuni ya Simba Logistics, alieleza kuwa alitokea nchini Congo DRC akiwa amepakia mzigo wa tani 32. Alipofika kwenye mzani wa Vigwaza, gari lake lilizuiliwa kwa madai ya kuzidi uzito.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Ulega alisema kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali zilifuata ushauri kutoka kwa menejimenti na wataalamu. "Pamela aliyekuwa akiendesha gari lenye namba T137 DLQ na trela lake T567CUR alilalamika kuhusu tabia na menendo yaliyojitokeza dhidi yake," alisema Ulega.
Ulega alifafanua kuwa hatua hizo ni pamoja na kuwasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo, na pia kuunda timu itakayochunguza tukio hili kuanzia mahali ambapo gari hilo lilipoingia nchini hadi kufika kwenye mzani wa Vigwaza ambapo tukio hilo lilitokea.
"Kwa lengo la kuwa na uchunguzi huru wa mwenendo wa tukio hili, pia tutatazama na mengine yanayoendelea katika mizani hiyo nchini. Timu hii itahusisha maofisa wa Serikali ambao tunaamini watafanya kazi kwa haki na kwa weledi mkubwa," aliongeza.
Aidha, Waziri Ulega alitoa maagizo kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kubadilisha mifumo ya uendeshaji wa mizani nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kama vile mifumo ya automatic, badala ya kuendelea na mfumo wa kibinadamu wa kujadiliana. "Watu waende na teknolojia za kisasa ili kuepuka migogoro ya aina hii," alisema.
Dereva Pamela alieleza zaidi kwamba mvutano huo ulianzia pale alipobisha kuhusu kuwa gari lake limepita mizani yote bila shida na kufika Vigwaza, ambapo aliambiwa gari lake limezidi uzito. "Walikataa kunisikiliza na walikushikilia bila huduma yoyote," alieleza.
Pamela alisema kuwa aliwasiliana na mwenye mali ili gari lipimwe tena, lakini watumishi wa mizani walisisitiza kuwa walikuwa sahihi. Aliongeza kuwa alikataa kulipa faini ya Sh. 956,400 kwa sababu aliona kuwa mzigo wake ulikuwa sawa na nyaraka alizozinazo.
"Nikamuita mwenye mali akaja na akawaambia wapime ili alipe faini wakasisitiza wao wapo sahihi na mimi nikahoji kwanini ni sahihi wakati mizani mingine nimepita kusiwe na tatizo hapa kwenu kuwe na tatizo?" alisema. "Hawakuweza kunisikiliza na nikachukua jukumu la kuomba vyombo vya habari vije vinisikilize ili nisikike na mamlaka kama Meneja wa Tanroads, Waziri na Rais asikie kilio cha madereva."
Pamela alisisitiza kuwa siyo mara ya kwanza kukutana na changamoto hizo kwenye mizani, akitaja kuwa katika safari yake kutoka Kongo, aliweza kupita mizani mbalimbali bila matatizo hadi alipofika Vigwaza. "Mimi malalamiko yangu ni kwamba nataka nipime mzani nijihakikishie kwa kuwa walichoniandikia sina uhakika nacho," alisema.
"Naomba Waziri watu wako wasikilize na kuangalia haki ya madereva kama mimi. Nisisitize kwamba sijakataa kulipa na sijaigomea mamlaka," alisema Pamela.
Akihitimisha, Pamela alieleza kuwa katika miezi miwili ya safari yake, kiongozi mmoja aliyejulikana kwa jina la Charles aliwahi kumkashfu na kumwambia kuwa kazi hizo ni za wanaume pekee, na kwamba wanawake wanapaswa kubaki nyumbani.
"Hii ni hali ambayo inadhihirisha ubaguzi na kutothaminika kwa madereva wanawake."
Waziri Ulega, kupitia hatua hizo, ameonesha dhamira ya kuhakikisha haki inatendeka na kuzuia matukio ya aina hii yasijirudie, huku akiendelea kuboresha mifumo ya mizani na kuhakikisha kuwa kila mmoja anapata haki yake bila upendeleo.

0 Comments:
Post a Comment