Viongozi zaidi ya 40 kutoka nchi mbalimbali za Afrika, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani cha ACT nchini Tanzania, Othman Masoud Othman, pamoja na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (CHADEMA), Tundu Lissu, wamezuiwa kuingia nchini Angola na mamlaka za serikali ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na chama cha ACT ilieleza kwamba, viongozi hao walizuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Luanda, ambapo hati zao za kusafiria zilikamatwa. "Viongozi hao wanashikiliwa kwenye uwanja wa ndege wa Luanda na hati zao za kusafiria zinashikiliwa," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Tundu Lissu, kupitia mtandao wake wa X (zamani Twitter), alieleza kuwa hatua hii ya mamlaka za uhamiaji za Angola haikubaliki na kwamba inapaswa kulaaniwa.
"Kilichofanywa na mamlaka za uhamiaji za Angola hakikubaliki na kinapaswa kulaaniwa," alisema Lissu.
Pia, Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, alithibitisha kupitia mtandao wake wa X kwamba aliandikishwa kushiriki katika tukio hilo na alikubaliwa na Rais wa UNITA, Adalberto Costa, lakini alizuiwa kuingia. "Tulialikwa na Rais wa UNITA, Adalberto Costa nchini Angola. Serikali imetuzuia kuingia," alisema Sifuna.
Viongozi wengine waliozuiwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Botswana, Ian Khama, Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine), kiongozi wa upinzani nchini Uganda, na wengine zaidi ya 40 kutoka bara la Afrika. Viongozi hawa walikuwa wamekusudiwa kushiriki katika mazungumzo ya siku nne kuhusu Demokrasia ya Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation, yaliyokuwa yaanze Machi 13 hadi 16, 2025.
Hadi sasa, mamlaka za serikali ya Angola hazijajitokeza kutoa maelezo yoyote kuhusu tukio hilo, licha ya juhudi za chama cha ACT na viongozi wengine kutaka ufafanuzi kutoka kwao.
0 Comments:
Post a Comment