Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kuongeza kwa kiwango kikubwa ushirikiano wao kwenye sekta ya ulinzi na wamekubali kuondoa vizuizi vya kibajeti ili kuwezesha serikali zao kuongeza matumizi ya kijeshi.
Ahadi hii ilitolewa jana wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji, hatua ambayo imechukuliwa baada ya miongo kadhaa ya kusuasua katika ushirikiano wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya.
Katika mkutano huo, nchi 26 za Umoja wa Ulaya zilitoa tamko la pamoja la mshikamano na Ukraine, licha ya Hungary kujitenga na kususia kutia saini nyaraka hiyo. Tamko hilo linatoa wazi nia ya Umoja wa Ulaya kuendelea kuiunga mkono Ukraine katika juhudi zake za kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi.
Hatua hii imechangiwa na wasiwasi unaoongezeka kwamba Marekani, mshirika mkuu wa nchi za Ulaya, inabadilika mwelekeo wake tangu kurejea madarakani kwa Rais Donald Trump, ambaye amerejea kusema kwamba nchi zisizotoa mchango wa kutosha kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO hazistahili kupewa ulinzi. Hali hii imeongeza shinikizo kwa Umoja wa Ulaya kujitegemea zaidi katika masuala ya ulinzi.
Kwa kuondoa vizuizi vya kibajeti, viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajia kuimarisha uwezo wao wa kijeshi na kuhakikisha kuwa nchi zao zinaweza kushirikiana zaidi katika masuala ya usalama wa kikanda na kimataifa.
0 Comments:
Post a Comment