Ugonjwa wa Mpox Wathibitishwa Nchini Tanzania, Serikali Yatoa Tahadhari

 


Tanzania imethibitisha kuwa kuna visa viwili vya ugonjwa wa Mpox, baada ya watu wawili kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huu. 


Hali hii imeibua wasiwasi kwa baadhi ya wananchi, huku Serikali ikiwa inatoa tahadhari na hatua za kujikinga ili kudhibiti maambukizi zaidi.



Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, watu hao wawili walibainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Mpox, zikiwemo vipele kwenye sehemu mbalimbali za mwili kama vile usoni, mikononi, na miguuni, pamoja na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, na maumivu ya viungo.

Uchunguzi wa maabara uliofanywa tarehe 9 Machi 2025, ulithibitisha kuwa wahisiwa hao wana maambukizi ya virusi vya Mpox. Mmoja wa waathirika ni dereva wa magari ya mizigo aliyesafiri kutoka nchi jirani kuelekea Dar es Salaam.

Katika taarifa yake, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema, “Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki.”

Mbali na maambukizi hayo, Mhagama alieleza kwamba chanzo cha ugonjwa wa Mpox ni virusi vinavyopatikana kwa wanyama wa jamii ya nyani. “Binadamu huweza kuupata ugonjwa huu kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi,” alisema.

Mpox, kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya virusi, haina tiba maalum, na hivyo mgonjwa hupewa matibabu kulingana na dalili alizonazo. Hata hivyo, serikali inaendelea na juhudi za kudhibiti ugonjwa huu kwa kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika maeneo yote ya nchi, ikiwemo maeneo ya mipakani.

Wizara ya Afya pia imehimiza wananchi kuchukua tahadhari muhimu za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu. Baadhi ya hatua zinazopendekezwa ni pamoja na:

  1. Kuwahi katika vituo vya huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapojisikia dalili za ugonjwa wa Mpox.
  2. Kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox, kama vile mikono, kubusiana, au kukumbatiana.
  3. Kuepuka kushiriki vitu vya matumizi binafsi kama vile mavazi na vifaa vya mwili vya mtu mwenye dalili za ugonjwa.
  4. Kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vitakasa mikono.

Wizara ya Afya imesema kuwa itatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na inashauri wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa kuzingatia tahadhari zinazotolewa.

Aidha, Mhagama alikumbusha kuwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg umeendelea kudhibitiwa na hadi sasa hakuna mgonjwa mpya. Serikali inasisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa ili kuhakikisha usalama wa afya yao na jamii kwa ujumla.


0 Comments:

Post a Comment