MOI Yaanza Upasuaji wa Kisasa wa Uti wa Mgongo kwa Njia ya Matundu



Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeweka historia kwa kuwa kituo cha kwanza nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoa huduma za upasuaji wa uti wa mgongo kwa njia ya matundu (Spine Endoscope). 


Huduma hii ya kisasa inalenga kuongeza ufanisi wa upasuaji, kupunguza makali ya maumivu kwa wagonjwa, na kufupisha muda wa kulazwa hospitalini.


Hatua hii imefanikishwa baada ya MOI kupokea mashine ya kisasa ya kufanyia upasuaji huo (Endoscope Tower) yenye thamani ya Shilingi milioni 500 kutoka kampuni ya Joimax ya Ujerumani. Kupatikana kwa mashine hii kutaifanya MOI kuwa kitovu cha huduma za upasuaji wa uti wa mgongo kwa njia ya matundu katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati, na Kusini, huku pia ikichagiza sekta ya tiba utalii.



Akizungumza leo Februari 5, 2025, wakati wa kambi maalum ya matibabu ya kibingwa ya uti wa mgongo ambapo wagonjwa 12 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema huduma hii mpya itabadilisha kwa kiasi kikubwa matibabu ya uti wa mgongo nchini.


"MOI imekuwa Taasisi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwa na kifaa hiki cha kisasa cha upasuaji wa mgongo kwa kutumia matundu. Ufanisi wa upasuaji utaongezeka na wagonjwa watapona haraka, hivyo kupunguza muda wa kukaa wodini," amesema Dkt. Mpoki.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, Dkt. Lemeri Mchome, amesema huduma hiyo mpya itakuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa kwani inasababisha majeraha madogo wakati wa upasuaji.


"Awali, MOI ilikuwa ikifanya upasuaji kwa kufungua eneo kubwa, jambo ambalo lilimlazimu mgonjwa kukaa muda mrefu wodini akiuguza jeraha na kumuacha na kovu kubwa. Mgonjwa alikuwa analazwa kwa siku tano au zaidi kutokana na ukubwa wa jeraha, na maumivu yalikuwa makali. Lakini kwa kutumia mashine hii, changamoto hizo zote zitakuwa historia," amesema Dkt. Lemeri.

Naye Dkt. Osama Nazar Kashlan, mkufunzi wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Weill Cornell cha Marekani, amepongeza MOI kwa kuwa tayari kuwekeza katika ujuzi wa watumishi wake na kuboresha huduma za kibingwa.

"MOI imeonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha weledi wa madaktari wake. Tutaendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo ili kuhakikisha wanakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya tiba duniani," amesema Dkt. Kashlan.

Huduma hii ya upasuaji wa uti wa mgongo kwa njia ya matundu ni hatua muhimu katika kuimarisha sekta ya afya nchini na kupunguza utegemezi wa wagonjwa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu ya aina hii.

Kupitia teknolojia hii mpya, MOI inajiimarisha kama kituo cha kibingwa katika matibabu ya magonjwa ya uti wa mgongo, jambo ambalo litaongeza imani ya wananchi kwa huduma za afya zinazotolewa ndani ya Tanzania. Vilevile, mafanikio haya yanafungua fursa kwa wataalamu wa afya wa ndani kupata mafunzo na uzoefu wa kisasa, hivyo kuinua viwango vya huduma za upasuaji nchini.

Kwa mafanikio haya, Tanzania inaelekea kwenye mapinduzi makubwa katika tiba za kibobezi, huku MOI ikiendelea kuwa kinara wa mageuzi haya katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati, na Kusini.


0 Comments:

Post a Comment