Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesema nchi yake inakubaliana na wazo la kusitisha mapigano na Ukraine, lakini hatua hiyo inapaswa kuleta "amani ya kudumu na kuondoa sababu za msingi za mzozo huu."
Putin aliyasema hayo wakati wa ziara ya mgeni wake, kiongozi wa Belarus, Alexander Lukashenko, akizungumza na waandishi wa habari.
"Nchi yetu inakubaliana na wazo la kusitisha mapigano, lakini ni muhimu kwamba hatua hii itoe amani ya kudumu na kuondoa sababu za msingi za mzozo huu," alisema Putin.
Awali, Kremlin ilisema kwamba iko katika hatua za mwisho za operesheni ya kuiondoa Ukraine kutoka maeneo ambayo iliteka huko Kursk.
Mjumbe wa Rais wa Marekani, Donald Trump, Steve Witkoff, yuko Moscow akiwakilisha Marekani katika mazungumzo yake na Urusi kuhusu pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30.
Putin alisisitiza umuhimu wa kuwa na utaratibu wa wazi kuhusu namna ya kusitisha mapigano. "Nani atatoa amri ya kusitisha mapigano, na amri hizi zitakuwa na thamani gani?" aliuliza Putin. "Nani ataamua ni wapi 'ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unawezekana kutokea' katika mpaka wa kilomita 2000?" akimaanisha urefu wa mpaka kati ya Urusi na Ukraine.
"Masuala haya yote yanahitaji kuchunguzwa kwa kina na pande zote mbili," aliongeza Putin, akisema kuwa wazo la kusitisha mapigano ni "zuri na tunaliunga mkono kabisa lakini kuna masuala yanayohitaji kujadiliwa."
Putin alisisitiza kuwa anahisi kuwa "tunapaswa kujadiliana na wenzetu wa Marekani na washirika wetu" na "pengine" atafanya mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani, Donald Trump.
"Wazo lenyewe la kumaliza mgogoro huu kwa njia za amani, tunaliunga mkono," alisema Putin.
0 Comments:
Post a Comment