Vatican City – Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, amelazimika kutumia tena mashine ya kupumulia baada ya kushindwa kupumua mara mbili siku ya Jumatatu alasiri, Vatican imeripoti.
Taarifa iliyotolewa na serikali kuu ya Vatican, Holy See, imesema: “Madaktari walilazimika kuingilia kati ili kuondoa kamasi kwenye mapafu ya Papa, lakini alikuwa macho na anajitambua wakati wote.”
Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, bado yuko chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari wake huku akisalia macho na kushiriki katika mazungumzo. “Baba Mtakatifu yuko macho, anajitambua na anatoa ushirikiano,” Vatican iliongeza.
Hali ya kiafya ya Papa imekuwa ikitilia wasiwasi waumini, hasa baada ya kulazwa hospitalini tangu Februari 14 kutokana na matatizo ya kupumua.
Awali, alitibiwa kikohozi kabla ya kugunduliwa na nimonia katika mapafu yote mawili.
Siku ya Ijumaa, alikumbwa na tukio jingine la kupumua kwa shida lililoambatana na kutapika, jambo lililoleta taharuki zaidi kuhusu hali yake.
Mamia ya Wakatoliki walikusanyika nje ya Uwanja wa St. Peter’s Square Jumatatu jioni kwa sala maalum za kumuombea kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki. Waumini wengi walionekana wakishika rozari mikononi mwao huku wakimuombea afya njema.
Hata hivyo, vyanzo kutoka Vatican vimeeleza kuwa hali ya Papa bado ni ngumu, na madaktari wake wanaendelea kumfuatilia kwa karibu.

0 Comments:
Post a Comment