NDUMBARO AAGIZA HATUA KUCHUKULIWA KWA WATUMISHI WANAOSABABISHA MIGOGORO YA WANANCHI

 


Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wa umma ambao wamekuwa chanzo cha migogoro kwa wananchi, hususan migogoro ya ardhi. 


Aidha, ameeleza kuwa kwa muda mrefu, unyanyasaji wa kijinsia umeonekana kama tatizo linalowakumba zaidi wanawake na watoto, lakini sasa hali imeanza kuonyesha sura mpya ambapo wanaume nao wanakumbwa na manyanyaso ya kijinsia. 



Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 53 ya watu waliopokea msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni wanaume, huku wanawake wakiwa asilimia 47.



Akizungumza jijini Arusha katika maonesho ya kuelekea kilele cha Wiki ya Wanawake Duniani, Waziri Ndumbaro alisema kuwa huduma hiyo ya msaada wa kisheria imeshatolewa katika mikoa 22 nchini na bado mikoa tisa. Alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amemtuma kwenda Arusha kushughulika na kero za wananchi, hasa zinazohusiana na migogoro ya ardhi na unyanyasaji wa kijinsia.


"Nimekuja kuweka kambi Arusha pamoja na timu ya wanasheria zaidi ya hamsini kutatua migogoro ya wananchi, na nikimaliza kuongea na nyinyi naanza kusikiliza kero zenu," alisema Ndumbaro.

Alibainisha kuwa serikali inachukua hatua kali dhidi ya watumishi wa umma wanaosababisha mateso kwa wananchi kwa makusudi, hasa wale wanaohusika na dhuluma ya ardhi na ukandamizaji wa haki.

Kero za Wananchi



Baadhi ya wananchi waliotafuta msaada wa kisheria ni pamoja na Padre Gabriel Ole Kilelo, mkazi wa Ngorongoro, ambaye alimweleza Waziri Ndumbaro namna Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro na maofisa wa ardhi walivyohusika katika kumnyang’anya maeneo yake. 


Alidai kuwa Mkurugenzi huyo alimnyang’anya ardhi yake licha ya yeye kutoa sehemu ya eneo lake bure kwa ajili ya huduma za jamii, akamzuia kupata wafadhili, na hata kumyima tenda za halmashauri kupitia shirika lake la Kidupo, linaloshughulika na elimu kwa watoto wa jamii ya kifugaji.

Alisema kuwa chanzo cha mgogoro wake na halmashauri hiyo ni juhudi zake za kuitetea serikali katika kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo, mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.



Kutokana na malalamiko hayo, Waziri Ndumbaro aliagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro na maofisa wa ardhi wilayani humo wafike katika banda la Katiba na Sheria siku inayofuata, Februari 5, 2025, kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo.

Mikoa Inayoongoza kwa Changamoto za Kisheria



Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, mkoa wa Geita umeongoza kwa changamoto nyingi za kisheria. Alisema kuwa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imewafikia watu zaidi ya milioni nane kwa njia ya elimu mtandaoni, huku zaidi ya watu milioni mbili wakihudumiwa moja kwa moja tangu mpango huo uanze mwaka 2023.


"Kigoma tuna changamoto ya uraia, huku katika mikoa mingine wananchi wengi waliojitokeza walikuwa na matatizo ya migogoro ya ardhi, mirathi, na unyanyasaji wa kijinsia," alisema Waziri Ndumbaro.


Aidha, alisema kuwa kati ya mikoa 22 iliyohudumiwa, migogoro mingi imehusu ardhi, ambapo wanawake wengi wanadhulumiwa, hasa kwenye mirathi.

"Sheria yetu iko vizuri kabisa, inatambua mchango wa kila mtu kwenye ndoa. Hata mwanamke au mwanaume ambaye hana kazi ana mchango wake. 


Shida kubwa ni pale ambapo mwanaume akifariki, maisha yanaendelea. Lakini mwanamke akifariki, hakuna tatizo. Lakini mwanaume akifariki, wanataka asirithi, wamtimue kwenye nyumba na asirithi mali. Hapo kuna changamoto kubwa sana," alifafanua Waziri Ndumbaro.

Ukandamizaji wa Kijinsia na Ukatili

Akizungumzia unyanyasaji wa kijinsia, Waziri Ndumbaro alisema kuwa katika baadhi ya maeneo, ndoa za utotoni bado ni tatizo kubwa. Alitoa mfano wa ndoa ya utotoni iliyovunjwa mkoani Shinyanga, ambapo msichana aliyekuwa amemaliza elimu ya sekondari alinusuriwa siku ya harusi na kurudishwa shuleni.

"Tulivamia harusini na kumnusuru mtoto ambaye sasa anamaliza kidato cha sita. Hii inaonesha jinsi kampeni hii ilivyo na umuhimu mkubwa kwa jamii yetu," alisema.

Kuhusu adhabu za ukatili wa kijinsia, Waziri alisema kuwa wakati wa ziara yake gerezani, baadhi ya wafungwa walilalamika kuwa adhabu ya miaka 30 kwa makosa ya ubakaji, ulawiti, na unyanyasaji ni kubwa.

"Niliwaambia kuna hoja bungeni, wanataka mkihukumiwa mkahasiwe. Niliwauliza kama wako tayari, wakasema hapana," alisema Waziri Ndumbaro.

Aidha, alisema kuwa suala la dhamana kwa makosa ya ukatili wa kijinsia linapaswa kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ili kuzuia wahalifu kuendelea kuhatarisha maisha ya waathirika.

"Haya masuala ya makosa ya ukatili wa kijinsia ni makubwa, inabidi tukaze nati. Maoni na hoja za wananchi zifike bungeni ili watu hao wasipewe dhamana kama ilivyo kwa makosa ya utakatishaji wa fedha haramu. Tunaona kwa sasa watu wanaanza kuyaogopa," alisema.

Mpango wa Kuendeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria katika Wizara ya Katiba na Sheria, Esther Msambaza, alisema kuwa mpaka sasa kampeni hiyo imeshafanyika kwenye mikoa 22, na wamebakiza mikoa tisa.

Alisema kuwa lengo la kampeni hiyo lilikuwa kuwafikia wanawake na kuwapa elimu kuhusu haki na wajibu wao katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kijamii, kiuchumi, na kisiasa.

"Wanaume wengi wanapojitokeza, migogoro yao inapohusisha familia, hutatuliwa kwa njia ambayo inaleta utulivu kwenye jamii. Hii inaonesha kuwa msaada wa kisheria una athari chanya kwa familia na jamii kwa ujumla," alisema Msambaza.

Aliongeza kuwa serikali inafanya mazungumzo na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili kuanzisha vituo vya kudumu vya Mama Samia Legal Aid katika mikoa mbalimbali, ili mpango huu uwe endelevu hata baada ya kipindi cha Rais Samia Suluhu Hassan.


"Tunapoondoka kwenye kila mkoa, tunaacha wanasheria wanaoendelea kutoa huduma. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata msaada wa kisheria kwa muda wote," alisema.


Kwa mujibu wa Waziri Ndumbaro, baada ya kukamilisha mikoa yote, kampeni hiyo itaelekezwa kwa wanamichezo ili kuhakikisha sekta zote zinaguswa na huduma hii muhimu.

0 Comments:

Post a Comment