Odinga, Ruto Wafanya Makubaliano ya Kisiasa: Azma ya Kuunganisha Kenya

 


Rais William Ruto wa Kenya na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga wameweka rasmi saini kwenye mkataba wa kisiasa, ishara ya azma yao ya kufanya kazi pamoja ndani ya serikali moja. 


Makubaliano haya kati ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Ruto na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga yamejikita katika kuhakikisha umoja wa kitaifa na kutatua changamoto kubwa zinazokikumba nchi.

Umoja wa Kisiasa

Katika tukio la kihistoria lililofanyika katika jumba la mikutano la KICC jijini Nairobi, makubaliano hayo yameonekana kuwa hatua muhimu katika siasa za Kenya. Makumi ya maelfu ya wafuasi wa vyama vya UDA na ODM walikusanyika kushuhudia mchakato huo, na huku wachanganuzi wakiona kwamba mkataba huu utaathiri uchaguzi mkuu ujao wa 2027.




Rais Ruto alisisitiza umuhimu wa umoja, akisema:
"Mimi namshukuru ndugu yangu Raila kwa kunishika mkono, tuungane badala ya kutengana, mkataba huu sio kwa manufaa ya mtu binafsi lakini kwa wakenya wote. Tuishi katika nchi ya umoja bila ya ubaguzi," aliongeza Rais Ruto.

Kwa upande wake, Raila Odinga aliungana na Ruto akisema:
"Leo tumeweka saini ya kuleta uelewano, amani na kupigana na maadui wa wakenya, mara hii tutatembea pamoja. Tunataka kuwaunganisha wakenya wote wawe kitu kimoja."

Changamoto na Mageuzi

Mkataba huo unalenga kuangazia masuala mbalimbali muhimu yanayoikumba Kenya, ikiwemo masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Rais Ruto alibainisha kuwa Kenya inapitia mabadiliko makubwa, na kwamba mabadiliko haya yanahitaji ushirikiano wa pande zote za kisiasa. Alisisitiza:
"Kenya inapitia mabadiliko makubwa, yanayoendeshwa na nguvu za utandawazi, teknolojia, na mabadiliko ya kijografia na hali ya hewa. Wakenya wanatarajia mageuzi makubwa yanayojumuisha kila mmoja."

Kwa mujibu wa mkataba huo, viongozi hao wawili wamekubaliana kutekeleza ripoti ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa ya NADCO, ambayo inahusisha kushughulikia gharama ya maisha, ajira kwa vijana, usawa wa kijinsia, na maendeleo shirikishi. Mkataba huo pia unahimiza mshikamano wa kisiasa na utawala unaojali usawa na fursa kwa wote.

Utekelezaji wa Ripoti ya NADCO

Miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa ni utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (NADCO). Ripoti hii iliibuka baada ya maandamano yaliyoandaliwa na wapinzani kufuatia uchaguzi mkuu wa 2022. Ripoti hiyo inajumuisha mageuzi muhimu ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya ajira kwa vijana na kupunguza gharama ya maisha.

Viongozi wa pande zote mbili walikubaliana pia kuimarisha ushirikishwaji wa makundi yote ya walio wachache, na kuboresha ugatuzi ili kuhakikisha kuwa huduma za kiserikali zinawafaidi wananchi katika ngazi ya mtaa.

"Mkataba huu unahusisha masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tunataka kuwa na serikali inayoleta haki na usawa kwa wote," alisema Odinga.

Vita Dhidi ya Rushwa na Uwajibikaji

Viongozi hawa pia walijitolea kwa pamoja kuhakikisha vita dhidi ya rushwa inafanikiwa kwa kuboresha taasisi zinazotekeleza uwajibikaji kama vile Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mdhibiti wa Bajeti. Aidha, suala la deni la taifa pia limejadiliwa kwa kubainisha haja ya kufanywa ukaguzi wa kitaifa ili kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanazingatia uwajibikaji.

"Tutaimarisha hatua za uwajibikaji ili kutathmini jinsi fedha zinavyotumika, na pia kuzuia upotevu wa rasilimali za serikali ili kuimarisha ufanisi," alisisitiza Rais Ruto.


Kwa pamoja, viongozi hawa wawili wameazimia kuleta mabadiliko ya kudumu nchini Kenya. Walikubaliana kuwa na uongozi wa kuzingatia uadilifu, kuhamasisha maendeleo ya sekta muhimu kama vile teknolojia na uchumi wa bluu, na kuhakikisha haki za wananchi zinaheshimiwa. Aidha, wameahidi kuwa watatoa fursa za ajira kwa vijana, ili kuimarisha ustawi wa taifa.

Mkataba huu unadhihirisha umoja wa kisiasa ambao unaweza kuleta mabadiliko chanya nchini Kenya, hasa katika kuelekea uchaguzi wa 2027.


"Tunahitaji kuwa na nchi yenye umoja na maendeleo kwa manufaa ya wote," aliongeza Raila Odinga.

0 Comments:

Post a Comment