Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Peter Msigwa, ameishukia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kusema kuwa hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi kwa kutumia hoja butu, huku akidai kuwa wanachama wa chama hicho wakiwa wamegawanyika.
Msigwa amemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kutekeleza ahadi zake za kampeni ya kuukwaa uenyekiti wa chama hicho.
Mchungaji Msigwa amesema hayo jijini Mbeya katika ziara ya siku tatu ya Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo Taifa, CPA Amos Makala, ikihusisha mikoa ya Mbeya na Iringa. Katika mkutano wa hadhara unaoendelea uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini hapa, Mchungaji Msigwa amewataka wananchi wasikubali kuingia kupinga uchaguzi.
“Hawana uwezo huo, hawana rasilimali watu, rasilimali fedha na wao wenyewe wamegawanyika. Mwenyekiti wao alisema anataka kufanya mabadiliko, moja ni ukomo wa uongozi bado hajafanya, ukomo wa viti maalum hawajafanya, wametoka kwenye uchaguzi wamegawanyika,” anasema Mchungaji Msigwa.
Amesema kuwa wakati alipohama CHADEMA alisema kuwa ndani ya chama hicho kuna ufisadi na hakuna demokrasia, na hadi sasa mambo hayo bado yapo. Mchungaji Msigwa alisisitiza kuwa ili kuwa na uhalali wa kusimama na kuishinikiza serikali kufanya mabadiliko, CHADEMA wanapaswa waanze na chama chao kwanza badala ya kuanzisha mapambano ya kuporosha Watanzania.
“Hawana sifa ya kutufundisha. Maendeleo ni mchakato na mabadiliko ni mchakato, kukomesha biashara ya utumwa ilichukua muda mrefu, hata miaka ya 50 na 60 wanawake walikuwa hawaruhusiwi kupiga kura wamedhalilishwa kwa karne nyingi,” alisema.
Aliongeza kuwa kubadilisha mtazamo huo imechukua muda, na kwamba hata mabadiliko katika nchi hii hayakuwa rahisi. “Si kweli kwamba CCM haijakubali mabadiliko, yako na yamefanyika makubwa,” alisema.
Msigwa aliendelea kusema kuwa CHADEMA hawana hati miliki ya kweli ya namna ya kuiendesha Tanzania, na kwamba hati hiyo inamilikiwa na Watanzania wote. Alieleza kuwa madai wanayoleta ni ya kutaka madaraka, lakini si ya kutatua matatizo ya wananchi.
“Huwezi kusikia wanazungumzia matatizo ya wananchi kwenye kilimo, afya, maboresho ya anga… hutawasikia wakizungumzia maboresho ya usafiri wa treni, watazungumzia namna ya kuingia madarakani,” alisema.
Mchungaji Msigwa alimaliza kwa kusema kuwa CHADEMA na vyama vingine vinajulikana kwa kupinga, lakini CCM kinajulikana kwa kazi inachofanya. Alisisitiza kuwa CCM itaendelea na kazi yake ya kuleta maendeleo kwa wananchi wote na kwamba mabadiliko halisi yataendelea kupatikana kupitia mchakato wa maendeleo na si kwa kupinga kila jambo.
0 Comments:
Post a Comment