'ACT Wazalendo Yatoa Wito kwa Serikali Kuwachukulia Hatua Viongozi wa CCM kwa Kupotosha U'ma Kuhusu Kuzuiliwa kwa Othman Masoud Othman Nchini Angola,
Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Makamu Mwenyekiti Bara, Stephen Wasira, na Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa CCM-Zanzibar, Hamis Mbeto, kwa tuhuma za kupotosha umma kuhusu tukio la kuzuiliwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, nchini Angola.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman mwenyewe, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Chama hicho, Magomeni, jijini Dar es Salaam. Othman alielezea kushangazwa kwake na matamshi ya viongozi wa CCM kuhusu tukio hilo na kudai kuwa upotoshaji huo umechangia kuibua wasiwasi kwa wananchi.
"Pomojna na taarifa zote zilizotolewa kuhusu tukio hili, watu wanapotosha juu ya jambo hili tena wanaofanya upotoshaji huu ni viongozi wa juu wa CCM, Makamu Mwenyekiti Wasira na Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa CCM-Zanzibar, Hamis Mbeto. Niseme wito wangu kwamba hasa kwa haya ambayo yamepotoshwa na watu ambao ni waandamizi wa Chama cha Mapinduzi, naiomba sana Serikali na natoa wito serikalini kama Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo kwamba Serikali iwachukulie hatua viongozi hao, kwa sababu upotoshaji wao umeipaka matope Serikali," alisema Othman.
Aliongeza kuwa, "Upotoshaji wao umewafadhaisha wananchi kwa kiasi kikubwa, wamefanya vitu kwa namna ambayo haiendani na nafasi zao, huo ndiyo wito wetu kama ACT."
Othman alifafanua kuwa kama kiongozi wa Serikali, kabla ya safari yake kwenda nchini Angola, alifuata taratibu zote zinazohitajika ikiwa ni pamoja na kuomba ruhusa kutoka kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi, ambaye alikubali na kumpa ruhusa kwa barua ya maandishi.
Kwa upande mwingine, Stephen Wasira, akizungumza katika mkutano uliofanyika Tunduma mkoani Songwe, alielezea kwamba viongozi wa ACT Wazalendo walikuwa wakielekea nchini Angola lakini walizuiliwa na paspoti zao kuchukuliwa. Wasira alisema: "Leo nimesoma viongozi walikuwa wanaenda Angola lakini wamenyang'anywa paspoti huko ni Angola sio hapa, hapa hatuja wanyang'anya paspoti na hata ikimaliza muda wake tunawapa, ili waende wanakotaka alafu warudi salama."
Wasira aliongeza kuwa, "Wamelalamika kwa nini Serikali imekaa kimya, kwani sisi tunasimamia Airpoti ya Angola? Airpoti ya Angola inasimamiwa na watu wa Angola, na pia huenda walikuwa na jambo lao ambalo wanalilitilia shaka, wangeuawa tungesema kwa nini wamewaonea watu wasiokuwa na hatia."
Vilevile, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, aliitaka Serikali kutoa hadharani sababu za kuzuiliwa kwa viongozi hao nchini Angola kwani hadi sasa haijatoa kauli rasmi kuhusu tukio hilo. Semu alieleza kuwa, "Serikali imekaa kimya na hawajatoa tamko lolote kuhusu tukio hili, ambayo imeacha maswali mengi miongoni mwa wananchi."
Semu aliongeza kuwa, "Tunaomba Serikali kumuita Balozi wa Angola nchini ili kutoa maelezo ya kina kuhusu sababu za tukio hili." Aidha, Semu alishauri Umoja wa Afrika (AU) kumteua Rais mwingine kuchukua nafasi ya uenyekiti wa AU, akisema kuwa Rais wa Angola ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa hawezi kuendelea na nafasi hiyo.
Viongozi wa ACT Wazalendo walizuiliwa kuingia nchini Angola mnamo Machi 2025 kushiriki katika mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD), yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation. Hadi sasa, Serikali ya Tanzania haijatoa kauli rasmi kuhusu tukio hilo.
0 Comments:
Post a Comment