DCEA YATEKELEZA OPERESHENI YA UTEKETEZAJI WA MASHAMBA YA MIRUNGI SAME

 


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi 2025. 



Katika operesheni hiyo, ekari 285.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa na watuhumiwa saba (7) wamekamatwa, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la mama Dangote.



Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema: "Mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria."


Kamishna Lyimo aliongeza kuwa, mwaka juzi Mamlaka ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na kilimo cha mirungi na badala yake wajikite katika kilimo cha mazao mbadala pamoja na ufugaji. Alisema: "Mwaka juzi tuliteketeza jumla ya ekari 535 za mashamba ya mirungi. Kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya, tulitoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya dawa za kulevya, ikiwemo mirungi. Lengo lilikuwa kuwawezesha wakazi wa eneo hili kujikita katika kilimo cha mazao mbadala na ufugaji kama njia ya kujiongezea kipato."


Aidha, Kamishna Lyimo alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, uongozi wa wilaya ya Same na Wizara ya Kilimo na Mifugo walitekeleza miradi ya ufugaji wa nguruwe na kugawa miche ya kahawa, iliki na mazao mengine kwa wananchi. Alisema: "Kutokana na juhudi hizo, wananchi wengi wameachana na kilimo cha mirungi na kuanza kulima mazao mbadala, japo wapo wananchi wachache waliokaidi na kuendelea na kilimo na biashara ya mirungi."


Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kufanya operesheni kuhakikisha wananchi wote wanaojihusisha na biashara ya mirungi wanakamatwa na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao. Alisema: "Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunatokomeza biashara na matumizi ya mirungi hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa, eneo hili la Same ni kitovu cha uzalishaji mirungi nchini hali inayohatarisha ustawi wa taifa letu ndio maana tunafanya operesheni hizi endelevu nchi nzima kuhakikisha tunadhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya za mashambani na viwandani ili zisiendelee kuathiri wananchi."


Kwa upande wake, Agness Mshana, mtendani wa kata ya Ekondi, alikiri kutambua uwepo wa watu wanaojihusisha na kilimo cha mirungi na kusema kuwa serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya mirungi. Alisema: "Tumejitahidi kuwaletea mradi wa nguruwe pamoja na miche ya miparachichi na kuwapa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa maana mirungi inamadhara mengi yakiwemo kuchanganyikiwa, kupoteza nguvu za kiume, kushindwa kuhudumia familia vizuri, kupata kansa na kadhalika."


Naye Bi. Hawa, mwananchi wa kata ya Tae wilaya ya Same, alisema kuwa, hajui sababu ya watu kuendelea kujihusisha na kilimo cha mirungi kwani, kuna mazao mengi yanayostawi kama vile vitunguu, karoti na iliki pamoja na miradi ya nguruwe iliyoletwa na serikali. Aliongeza: "Aidha, ameiomba serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa kupelekwa sokoni, hali itakayosaidia wananchi kuwa na uhakika wa masoko ya mazao yao na hivyo kuachana na biashara ya mirungi."


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wazalishaji, wasambazaji, na watumiaji wa dawa za kulevya. Ushirikiano huu utasaidia kutokomeza kabisa biashara hii haramu na kulinda ustawi wa jamii. Kamishna Lyimo alimalizia kwa kusema: "Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika ili kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa salama na lenye maendeleo endelevu."


0 Comments:

Post a Comment