CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtahadharisha Sigrada Mligo, ambaye ni kiongozi wa Uenezi wa Baraza la Wanawake, kuwa makini na uhusiano wake na Chama Cha Mapinduzi (CCM). CHADEMA kimeonya kuwa Sigrada anapaswa kuepuka kutumia uhusiano huo katika njia zinazoweza kuathiri si tu hadhi ya chama hicho, bali pia hadhi yake mwenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, CHADEMA inafuatilia kwa karibu kila hatua inayochukuliwa kuhusu tuhuma za kupigwa kwa Sigrada Mligo, zinazozagaa mitandaoni. Chama hicho kimesisitiza kuwa kinashirikiana na vyombo husika vya ndani na nje ya chama ili kuhakikisha uchunguzi wa tuhuma hizo unafanyika kwa uwazi na haki.
“CHADEMA kinafuatilia kwa karibu tuhuma zinazozungumziwa kuhusu kupigwa kwa Sigrada Mligo. Tutatoa taarifa rasmi kuhusu hali hii kadri itakavyohitajika na hali itakavyokuwa,” alisema Brenda Rupia.
Sigrada anadaiwa kupigwa Machi 25, mwaka huu, mkoani Njombe, na mmoja wa walinzi wa CHADEMA kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.
Hadi sasa, chama hicho kinadai kuwa kinaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na kitasubiri matokeo ya uchunguzi huo kabla ya kutoa taarifa kamili.
Kwa upande mwingine, chama hicho kimesisitiza kuwa haki itatendeka katika suala hili, na kwamba vitendo vya vurugu au vurugu zinazohusisha wanachama wake havikubaliki na vitachukuliwa hatua stahiki.
0 Comments:
Post a Comment