Vyama vya Upinzani Afrika Vyalaani Kitendo cha Angola Kuwazuia Viongozi wa Upinzani Kuingia Nchini

 


Kundi la vyama vya upinzani barani Afrika kupitia Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD), limetaja kitendo cha serikali ya Angola kuwazuia wanasiasa wakuu wa upinzani kutoka barani kote kuingia nchini humo kuwa ni shambulizi dhidi ya demokrasia.

Katika taarifa yao ya pamoja, vyama hivyo vimesema kitendo cha mamlaka za Angola kuzuia karibu viongozi 40 wakubwa wa upinzani kutoka nchi zaidi ya 20 ni kampeni ya kimfumo na ya kijinga ya kushambulia na kudhoofisha maendeleo kuelekea demokrasia na uwajibikaji barani Afrika.

Viongozi hao walizuiwa katika uwanja wa ndege wa Luanda, walipowasilia kushiriki katika mjadala wa siku nne wa Jukwaa la Demokrasia Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation, ambayo yalianza Machi 13 na yatakamilika Machi 16.

Baadhi ya viongozi waliozuiwa, wakiwa ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, ambaye amelaani kitendo hicho akisema: "Kitendo kile ni shambulio dhidi ya Diplomasia na Demokrasia Afrika."

Mbali na Masoud, aliyekuwa rais wa Botswana, Ian Khama, Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho, Moeketsi Majoro, Rais wa zamani wa Colombia, Andrés Pastrana Arango, na wapinzani wengine 24 walishikiliwa kwa zaidi ya saa 9 katika uwanja wa ndege.


Wapinzani wengine waliozuiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani cha Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, Kiongozi wa upinzani Uganda, Robert Kyagulanyi (Bobi Wine), na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna.

Baadhi ya viongozi wamerudishwa katika nchi zao kabla ya baadaye kuruhusiwa kuingia nchini Angola.


Mamlaka za Angola zimesema kilichotokea kinahusiana na masuala ya uhamiaji na utaratibu wa vibali vya kuingia nchini humo vilivyopaswa kufuata utaratibu wa sheria.

0 Comments:

Post a Comment