Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, imepitisha mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za Uteuzi wa Wagombea Uongozi katika Vyombo vya Dola na kuanzisha ukomo wa viti maalum kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Marekebisho haya ni sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia na uongozi bora ndani ya chama yamefanyika katika mkutano maalum uliofanyika tarehe 10 Machi, 2025, jijini Dodoma,
Kama ilivyoainishwa katika taarifa ya Katibu wa NEC, Idara ya Organizesheni, Issa Haji Ussi, iliyotolewa tarehe 11 Machi, 2025, CCM imeweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano kwa nafasi za ubunge, uwakilishi, na udiwani wa viti maalum wanawake.
Ukomo huu utaanza kutumika rasmi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030.
Hatua hii ni muhimu kwa kutoa nafasi kwa viongozi wapya kuingia katika vyombo vya dola na kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika uongozi.
Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi: Kuboresha Mchakato wa Uchaguzi
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa imepitisha marekebisho ya Kanuni za Uteuzi wa Wagombea Uongozi. Mabadiliko haya yanahusisha mchakato wa uchujaji na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi wa majimbo, na udiwani wa kata, pamoja na viti maalum wanawake. Katika taarifa iliyotolewa, Issa Haji Ussi alieleza kuwa mchakato huu utaimarisha demokrasia na uwazi, huku ukipanua uwakilishi wa wanachama wa CCM katika mchakato wa uteuzi.
Kwa mfano, kwa upande wa mchakato wa uteuzi wa wanawake katika Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT), wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa UWT wa Mkoa watakuwa na jukumu la kutoa maoni kwa uteuzi wa wagombea, jambo ambalo linalenga kuimarisha ushirikishwaji wa wanachama katika kila ngazi ya chama.
Kauli Mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa 2025: "Kazi na Utu, Tunasonga Mbele"
Halmashauri Kuu ya CCM pia imepitisha kauli mbiu rasmi kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025. Kauli mbiu hii inasema: "KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE".
Kauli mbiu hii inaakisi dhamira ya CCM ya kuendeleza juhudi za ujenzi wa Taifa lenye maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa, na ustawi wa watu wenye kujali utu. Kauli mbiu hii inatarajiwa kutoa msukumo mkubwa kwa wananchi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, huku ikisisitiza umuhimu wa kazi, utu, na maendeleo kwa jamii.
Marekebisho ya kanuni za uteuzi, pamoja na hatua ya kuweka ukomo wa viti maalum kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, ni hatua muhimu inayolenga kuongeza uwazi, usawa, na uwakilishi katika mchakato wa uchaguzi. Huu ni mchakato endelevu wa kuimarisha demokrasia na kutoa nafasi kwa viongozi wapya kuingia katika vyombo vya dola. Kwa kuzingatia kauli mbiu ya uchaguzi ya "Kazi na Utu, Tunasonga Mbele", CCM inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo na ustawi wa wananchi wote.
0 Comments:
Post a Comment