Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) imefanikisha lengo lake la kutoa huduma ya majisafi kwa asilimia 99 kwa wakazi wa Jiji la Arusha, kupitia miradi mbalimbali ya maji na majitaka.
Huu ni mafanikio makubwa katika sekta ya maji, na ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za maji kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba, alieleza mafanikio haya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, tarehe 14 Machi 2025, jijini Dodoma. Mhandisi Rujomba alisema, "Eneo la Jiji la Arusha kwa kupitia Mradi mkubwa, AUWSA imefanikisha upatikanaji wa majisafi kwa asilimia 99."
Aidha, alisema kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, AUWSA imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali za kuboresha huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka kwa wakazi wa Jiji la Arusha zitakazogharimu jumla ya shilingi bilioni 4.2.
"Mamlaka itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kufanikisha adhma ya kuhakikisha huduma za majisafi na usafi wa mazingira zinaboreshwa kwa maendeleo endelevu ya Jiji la Arusha na maeneo ya pembezoni," alisema Mhandisi Rujomba.
Miradi hiyo ni pamoja na kutekeleza mradi wa maji Shangarai, kukamilisha mradi wa maji Kiranyi-Ngateu, kupanua mtandao wa majisafi urefu wa kilomita 76 ili kuunganisha wateja 14,000 kwa mwaka, kuboresha mtandao wa majitaka kwa fedha za ndani kwa kilomita 10, kuongeza wateja 1,000 wa majitaka, na ujenzi wa ofisi mpya ya Kanda ya Monduli.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Rujomba alitoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Serikali imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji ambayo yameleta athari chanya kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha.
Kwa upande wa huduma ya majitaka, Mhandisi Rujomba alisema AUWSA imefanikiwa kupanua mtandao wa kukusanya majitaka kutoka asilimia 8.03 (2020/21) hadi asilimia 39.5 mwaka 2024/25. Pia, alifafanua kuwa majitaka yanayokusanywa kutoka kwa wateja zaidi ya 10,930 yanatibiwa katika mabwawa ya kutibu majitaka yaliyopo Terrat (Themi Holding Ground) na baada ya kutibiwa, maji hayo yanawanufaisha wananchi walipo kusini mwa mabwawa hayo kwa shughuli za kiuchumi kama kilimo cha umwagiliaji.
Mhandisi Rujomba pia alizungumzia uboreshaji wa huduma za maji, akisema kwamba masaa ya upatikanaji wa huduma ya maji yameongezeka kutoka saa 16 (2020/21) hadi saa 22 mwaka 2024/25. Idadi ya wateja waliounganishwa na huduma za maji imeongezeka kutoka 71,183 (Juni 2021) hadi 134,000 kwa sasa.
Kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), AUWSA imekamilisha mradi mkubwa wa maji kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa majisafi na kuboresha huduma ya uondoaji wa majitaka katika Jiji la Arusha.
Miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na AUWSA ni pamoja na Mradi wa Majisafi Mlangarini, Mradi wa uondoaji wa majitaka A–Z, Mradi wa Majisafi Imbaseni, Mradi wa Majisafi Enguik–Monduli, Mradi wa Majisafi Vijiji Nane–Ngorongoro, na Mradi wa Vijiji Saba–Arumeru.
Miradi hii inatarajiwa kuimarisha zaidi huduma za maji na usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha na vitongoji vyake, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo haya.






0 Comments:
Post a Comment