Benki Kuu ya Tanzania imebainisha kuwa taarifa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kushindwa kufungua akaunti za benki na kulazimika kufuata kadi zao nchini hazina ukweli.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tútuba, amesema kuwa ufuatiliaji uliofanywa na benki kuu katika benki za hapa nchini umeonyesha kwamba taratibu za huduma kwa wateja wa Diaspora ni rafiki na za haraka.
"Taratibu zilizopo kwa wateja wa Diaspora ni rafiki na za haraka. Katika kuhakikisha kuwa Diaspora wanapata huduma kwa wakati, benki husika zimefungua madawati mahsusi ya kuwahudumia wateja hao na nyingine zimeanzisha vifurushi maalumu vya Diaspora," alisema Gavana Tútuba.
Aidha, Gavana Tútuba alieleza kuwa ili kufungua akaunti, mteja anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au hati ya kusafiria. Vitambulisho hivyo vinaweza kuwasilishwa kwenye dawati la benki husika au kutumwa kwa njia ya mtandao kwa ajili ya kufanyiwa kazi. "Baada ya akaunti kufunguliwa, mteja ana uhuru wa kuchukua kadi yake mwenyewe kwa kwenda kwenye benki husika endapo yupo hapa nchini, au kuielekeza benki yake namna anavyotaka kutumiwa kadi hiyo ili imfikie mahali aliko," alisisitiza.
Kwa upande mwingine, Gavana Tútuba alisisitiza kuwa benki Kuu ya Tanzania inaunga mkono jitihada za Serikali za kuwahimiza Diaspora wa Tanzania kuwekeza nchini kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa taifa. "Benki Kuu itaendelea kufuatilia na kuhakikisha kwamba mteja mwenye changamoto mahsusi kwenye benki yoyote anatatuliwa na kupewa huduma za kibenki kwa ukamilifu na haraka," aliongeza.
Gavana alihimiza benki za biashara kuendelea kutoa elimu kuhusu huduma zao kwa wananchi wote, wakiwemo Diaspora wa Tanzania, ili waweze kufahamu taratibu zinazotakiwa kufuatwa na kupata huduma stahiki kwa wakati bila changamoto.

0 Comments:
Post a Comment